2016-08-04 08:01:00

Vijana wameshuhudia nguvu ya ujasiri inayofumbatwa katika huruma!


Vijana wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè wameshiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani huko, Cracovia, Poland iliyokuwa inaongozwa na kauli mbiu “Heri wenye rehema maana hao watapata rehema”. Vijana wameonesha na kushuhudia kwamba, inawezekana kukita maisha katika ujasiri wa huruma ili kujenga na kudumisha urafiki na udugu kati ya vijana wa kizazi kipya.

Vijana wanapaswa kuwa kweli ni vyombo, mashuhuda na mitume wa huruma ya Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu, kwani wanao uwezo na jeuri ya kutenda yote haya kwa ari na moyo mkuu anasema Fra Alois, Mkuu wa Jumuiya ya Kiekumene ya Taizè. Baba Mtakatifu amewagusa vijana na kujitahidi kuzima kiu ya maisha yao ya kiroho wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Poland. Amewapatia changamoto ya kusimama kidete kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa kutambua kwamba, wao ni nguvu na chachu ya mabadiliko katika ulimwengu mamboleo.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 yamejikita kwa namna ya pekee katika dhana ya huruma ya Mungu na vijana wamepata nafasi nchini Poland kutembelea, kujionea na kuzamishwa katika bahari ya huruma ya Mungu kama ilivyoasisiwa na Watakatifu Yohane Paulo II na Sr. Faustina Kowalska, mtume wa Ibada ya huruma ya Mungu duniani. Maadhimisho haya yamekwenda sanjari na Mwaka wa huruma ya Mungu, ili kuwakumbusha vijana kwamba, hata katika ulimwengu utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia bado wanahitaji kujikita katika tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili, kama chachu ya ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake!

Vijana wameguswa na kutikiswa kwa namna ya pekee kutokana na vitendo vya kigaidi vinavyoendelea kusikika sehemu mbali mbali duniani, kiasi cha kuwakatisha tamaa ya maisha na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Baba Mtakatifu Francisko amewajengea vijana ujasiri wa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha tunu msingi za maisha kwa kujikita katika haki na amani; umoja na udugu; upendo na mshikamano wa dhati; mambo yanayomwilishwa katika majadiliano ya kidini na kiekumene, ili dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Ulimwengu mamboleo unakabiliana na changamoto za wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, ukosefu wa haki na amani, vitendo vya kigaidi; athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa. Matukio yote haya yanahatarisha hija ya matumaini miongoni mwa familia ya Mungu duniani, kumbe, watu hawana budi kupiga moyo konde na kusonga mbele kwa imani na matumaini katika mchakato wa ujenzi wa: haki na amani; umoja na mshikamano kati ya watu pasi na ubaguzi.

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani imekuwa ni fursa ya kuwaunganisha vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia ili kusherehekea zawadi ya imani inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Poland imeonesha kwamba ni nchi ambayo imani inashuhudiwa katika uhalisia wa maisha na kwamba, ni kwa njia ya imani, familia ya Mungu nchini Poland imeweza kuvuka vikwazo na majaribu makubwa katika maisha yake, leo hii ni mfano bora wa kuigwa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.