2016-08-04 14:43:00

Simameni kidete kupambana na ugaidi na jengeni umoja wa kitaifa


Dini zote duniani zina dhamana ya kuhakikisha kwamba zinasimama kidete kupambana na vitendo vyote vya kigaidi pamoja na misimamo mikali ya kidini, ili kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa. Viongozi wa kidini wanapaswa kuhakikisha kwamba, wanasimamia mafundisho sahihi ya imani yao kwa kukazia uhuru wa kuabudu, haki msingi za binadamu, utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Haya ni mambo msingi yaliyopewa kipaumbele cha pekee na viongozi wa kidini nchini Tanzania waliokutana hivi karibuni mjini Dodoma ili kujadili kwa kina na mapana mchango wa dini katika mapambano dhidi ya vitendo vya kigaidi na mipasuko ya kijamii kutokana na misimamo mikali ya kiimani. Majaribio na vitendo vya kigaidi ni tafsiri potofu ya Vitabu vitakatifu. Kumbe, waamini wanapaswa kusaidiwa kuwa na mwelekeo sahihi kuhusu mafundisho ya imani yao, ili kukuza na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Askofu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo Katoliki Bunda alishiriki katika mkutano huu kwa niaba ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania ambaye amekazia pamoja na mambo mengine, umuhimu wa viongozi wa kidini kutoa mafundisho sahihi ya imani yao sanjari na kuwa na tafasiri sahihi ya Vitabu vitakatifu sanjari na kujenga umoja na mshikamano kati ya watu. Lakini kwa bahati mbaya, kuna baadhi ya viongozi wa kidini wameshindwa kutekeleza dhamana ya kuwafunda vyema waamini wao, kiasi kwamba waamini nao wamepoteza dira na mwelekeo wa maisha ya kiroho na matokeo yake ni ukavu wa kiroho.

Askofu Kwande anawahimiza viongozi wa kidini kuhakikisha kwamba, wanajikita katika kuwafunda waamini wao mambo msingi ya kiimani kadiri ya Vitabu vitakatifu; lakini ushuhuda wa maisha adili na matakatifu ni mfano bora zaidi wa kuigwa. Kwa upande wake, Alhaji Mussa Salum kutoka Dar es Salaam amekazia umuhimu wa kutunza na kuendeleza misingi ya amani na utulivu. Baadhi ya waamini wa dini ya Kiislam anasema, wanashutumiwa kwa kuwa na misimamo mikali ya kidini pamoja na kushiriki katika vitendo vya kigaidi ni kutokana na kukosekana kwa tafsiri na mafundisho makini ya dini ya Kiislam.

Itakumbukwa kwamba, dini ya Kiislam ni dini ya amani na wala si dini inayojikita kwenye vitendo vya kigaidi. Maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kusimama kidete kulinda na kudumisha tunu ya maisha ni sehemu ya mafundisho ya dini ya Kiislam na kwamba, vitendo vya kigaidi ni jambo ambalo halikubaliki hata kidogo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.