2016-08-04 15:28:00

Imarisheni utume kwa vijana, ili wawe mashuhuda wa huruma ya Mungu!


Maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 yaliyoongozwa na kauli mbiu “Heri wenye rehema maana hao watapata rehema” imekuwa ni fursa kwa vijana wa kizazi kipya kujizamisha katika bahari ya huruma ya Mungu, ili hatimaye, waweze kujichotea chemchemi hii inayopaswa kumwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. 

Padre Wojciech Adam Koscielniak kutoka katika Kituo cha Hija cha Kiabakari Jimbo Katoliki Musoma katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, vijana wameshuhudia chemchemi ya huruma ya Mungu iliyoyokuwa inabubujika kutoka kwa Mtakatifu Faustina Kowalska, ambaye katika ujana wa miaka 33 alionja mateso na majaribio mbali mbali lakini kwa msaada wa neema na huruma ya Mungu akua na kukomaa katika ujana wake, leo hii ni shuhuda na mtume wa Ibada ya huruma ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu sanjari na Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 iwe ni fursa kwa vijana kuzamisha huruma ya Mungu katika maisha na vipaumbele vyao, badala ya kujitafuta wenyewe kwa njia ya mitandao ya kijamii. Vijana wajitahidi kuwa ni mashuhuda, vyombo na mitume wa huruma ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku, lakini zaidi miongoni mwa vijana wenzao, ili kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuwainjilisha vijana wa kizazi kipya kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Vijana wanahamasishwa kuondokana na ubinafsi na uchoyo ili waweze kuwa tayari kujenga familia ya Mungu inayowajibika na kutaabikiana. Vijana wawe ni vyombo na mashuhuda wa wema, upendo na huruma ya Mungu kwa watu wa mataifa. Dhana ya huruma ya Mungu iwasaidie vijana kujipokea, kujikubali, kujisahihisha na kujirekebisha ili waweze kuwa ni watu wema zaidi sanjari na kuwapokea vijana wenzao jinsi walivyo kwa kuwapatia nafasi ya kukua na kukomaa katika maisha na utu wao.

Padre Wojciech Adam Koscielniak anakaza kusema, vijana wanapaswa kujikita katika huruma ya Mungu, ili iweze kuwa ni sementi ya huruma na upendo kwa Mungu na jirani, tayari kukoleza Uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili pamoja na utume kwa vijana wa kizazi kipya. Maadhimisho haya yasaidie kukoleza ari na moyo wa kufufua vyama vya kitume miongoni mwa vijana kwani vyama hivi visipowekewa mpango mkakati wa shughuli za kichungaji, baada ya muda si mrefu, hatitakuwepo tena.

Vijana waimarishe: TYCS, Viwawa na vyama vingingine vya kitume miongoni mwa vijana na kwa njia ya utume kwa vijana waweze kuthubutu kutubu, kuongoka na kumrudia tena Mwenyezi Mungu katika maisha yao, kwa kujenga na kujikita katika mahusiano mema na Mungu pamoja na jirani zao, ili kuimarisha utume wa vijana wenye tija na mashiko! Vijana wasipokuwa vyombo, mashuhuda na mitume wa huruma ya Mungu, dunia itawaka moto kwa majanga yasiyokuwa na kifani, lakini huruma ya Mungu inawasaidia vijana kujenga umoja, amani, upendo na mshikamano wa dhati na jirani zao. Kumbe, vijana wanapaswa kuwa na huruma kama Baba wa mbinguni anakaza kusema Padre Wojciech Adam Koscielniak kutoka Kituo cha Hija cha Kiabakari, Jimbo Katoliki Musoma katika mahojiano maalum na Radio na Radio Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.