2016-08-04 07:19:00

Damu ya Padre Jacques Hamel iwe ni chachu ya haki na amani!


Waamini wa dini na madhehebu mbali mbali na wapenda haki, amani na maridhiano kati ya watu,  Jumanne, tarehe 2 Agosti 2016 wameshiriki kwa wingi katika Ibada ya Misa ya Mazishi ya Padre Jacques Hamel, mwenye umri wa miaka 85 aliyeuwawa kikatili, wakati akiadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Parokia Mtakatifu Etienne – du Rouvray, huko Ufaransa na magaidi wawili.

Waamini wa dini ya Kiislam, Jumapili iliyopita walionesha mshikamano wa upendo na maridhiano kwa kushiriki sala ya pamoja katika Makanisa ya Kikristo yaliyoko karibu nao, ili kuonesha kwamba, inawezekana waamini wa dini mbali mbali wakaishi kwa amani, upendo na utulivu, huku wakiheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti zao za kidini. Tukio hili limepongezwa na wapenda amani duniani kwamba, ni hatua kubwa katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini kati ya waamini wa dini mbali mbali hasa nchini Ufaransa ambako vitendo vya kigaidi vinaendelea kusababisha mipasuko ya kidini na kiimani miongoni mwa wananchi.

Matukio yote haya yawe ni chachu ya maridhiano, haki, amani, upendo na mshikamano kati ya watu. Marehemu Padre Jacques Hamel angaliwapenda wote kama walivyokuwa wamefurika kwenye Ibada ya maziko yake pasi na tofauti wala utengano wa kidini, kiimani au rangi ya mtu! Hivi ndivyo alivyosikika akisema Askofu mkuu Dominique Lebrum, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Rouen, Ufaransa wakati wa mahubiri yake, kwa kusema kwamba, wote waliohudhuria mazishi ya Padre Hamel kwa namna ya pekee walikuwa wanaunda familia ya Padre Jacques.

Huyu ni Padre aliyekuwa na uchaji mkubwa kwa Mungu, akashuhudia imani yake kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili, changamoto na mwaliko kwa walimwengu kujenga na kudumisha mshikamano wa haki, amani na upendo, ili kuondokana na utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika chuki, uhasama na hali ya kulipizana kisasi. Ikumbukwe kwamba, haki na amani ni tunu msingi katika ujenzi wa mafungamano na maendeleo ya kijamii. Kuna maelfu ya watu wanaoendelea kupoteza maisha kutokana na vita, vitendo vya kigaidi, nyanyaso na dhuluma za kidini. Ifike mahali walimwengu waseme, tumechoka kusikia litania za maombolezo ya watu waliofariki dunia, sasa tunataka kuona haki, amani na maridhiano kati ya watu vikitalawa!

Dhambi na ubaya wa moyo ni mambo yanayomsababishia mwanadamu kwenda nje kabisa ya utu na ubinadamu wake. Huu ni mwaliko wa kupambana na shetani kama alivyosikika akisema Padre Jacques, ondoka kwangu we shetani, akaanguka chini na kukata roho! Hapa alikiri imani yake kwa Mwenyezi Mungu muumba wa vyote vinavyoonekana na visivyoonekana; akashuhudia imani kwa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu, lakini binadamu ambaye amejikuta akiogelea katika dimbwi la ubaya na dhambi kutokana na hila za shetani. Ndiyo maana Yesu katika maisha na utume wake, alipandana bila kuchoka na hila za shetani, akawataka wafuasi wake kuwa macho zaidi. Kwa neema na baraka za Mwenyezi Mungu, watu wanaweza kutubu na kumwongokea Mungu, wakabadili nia zao mbaya na kuanza mchakato wa maisha mapya, huku wakimwachia nafasi Mwenyezi Mungu ili aweze kuwaundia moyo safi ili kuambata Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Askofu mkuu Dominique Lebrum ametumia nafasi hii kuwaombea wale wote waliokuwa wamefungwa katika kongwa la utumwa wa shetani kwa kuwa na chuki, uhasama na vitendo vua kigaidi, ili waweze kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo. Waamini wanaalikwa wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria kupalizwa mbinguni, hapo tarehe 15 Agosti 2016 watakapokuwa Makanisani wawache mshumaa kwa nia ya kumwombea Marehemu Padre Jacques Hamel pamoja na kuombea haki, amani na maridhiano kati ya watu. Watu wajenge na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati pasi na chuki wala uhasama, kazi inayotekelezwa na adui shetani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.