2016-08-03 07:15:00

Hayati Kardinali Macharski: Yesu ninakutumainia!


Baba Mtakatifu Francisko anaungana na familia ya Mungu nchini Poland kuomboleza kifo cha Kardinali Franciszek Macharski, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Cracovia aliyefariki dunia akiwa na umri wa miaka 89 hapo tarehe 2 Agosti 2016 baada ya kuugua kwa muda mrefu. Baba Mtakatifu Francisko alipokuwa nchini Poland alipata nafasi ya kwenda kumtembelea hospitalini alikokuwa amelazwa akiwa katika hali mbaya sana.

Baba Mtakatifu katika salam zake za rambi rambi kwa Kardinali Stanislaw Dziwisz, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cracovia anasema, anapenda kumshukuru Mungu kwa zawadi ya maisha, dhamana na wito aliomkirimia Hayati Kardinali Macharski, mhudumu mwaminifu wa Injili ya Kristo aliyejiaminisha mbele ya Kristo, kama dira na mwongozo wa maisha na utume wake. Kauli mbiu “Yesu ninakutumainia wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, umekuwa ni utenzi wa sifa kwa matendo makuu ambayo Mwenyezi Mungu ameyatekeleza katika maisha yake tangu katika ahadi ya Ubatizo, alipomuunganisha na kundi la waja wake waliokombolewa kwa Damu Azizi ya Kristo Mkombozi wa dunia; akamjalia zawadi ya Daraja Takatifu, ili kuwatakatifuza watu wa Mungu kwa njia ya Neno na neema za Sakramenti za Kanisa.

Marehemu Kardinali Macharski alitekeleza utume wake kwa ari na moyo mkuu kama: Mchungaji, Jaalimu, Gombera hadi pale alipoteuliwa kukalia kiti cha Mtakatifu Stanislaw, Jimbo kuu la Cracovia, mara tu baada ya Karol Wojtyla kuteuliwa kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro, leo hii ni Mtakatifu Yohane Paulo II. Marehemu Kardinali Macharski kwa kujiaminisha katika huruma ya Mungu, alipokea utume wake kama Baba wa Wakleri na waamini wakawa na imani katika huduma zake za kichungaji.

Alifanikiwa kuliongoza Jimbo kuu la Cracovia katika kipindi kigumu cha mageuzi ya kisiasa na kijamii; akaonesha hekima na busara katika uhalisia wa mambo; akasimama kidete kulinda na kudumisha utu na heshima ya kila mtu; ustawi na mafao ya Kanisa, lakini zaidi katika kuhifadhi imani nyoyoni mwa watu! Baba Mtakatifu Francisko anamshukuru Mungu aliyemwezesha kupata fursa ya kumtembelea hospitalini alikokuwa amelazwa mahututi huko Cracovia. Katika siku zake za mwisho wa maisha yake alijaribiwa sana, akaendelea kuwa mwaminifu na shuhuda ya wema na huruma ya Mungu. Hii ndiyo kumbu kumbu anasema Baba Mtakatifu ambayo imechapwa katika akili na kwenye sala zake. Anamwombea Mwenyezi Mungu ili aweze kumpokea katika maisha ya uzima wa milele. Baba Mtakatifu Francisko anawapatia wote walioguswa na msiba huu mzito baraka zake za kitume!

Hayati Kardinali Franciszek Macharski, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Cracovia alizaliwa kunako tarehe 20 Mei 1927. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, kunako tarehe 2 Aprili 1950 akapewa Daraja Takatifu la Upadre. Kunako mwaka 1956 alihamishiwa nchini Uswiss kuendelea na masomo ya juu katika uwanja wa taalimungu na kufanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika masomo ya taalimungu ya shughuli za kichungaji. Kwa muda wa miaka 10 akafundisha somo hili kwenye Chuo kikuu cha Cracovia na kunako mwaka 1970 akateuliwa kuwa Gombera wa Seminari kuu ya Cracovia.

Papa Yohane Paulo II kunako tarehe 29 Desemba 1978 akamteuwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cracovia na kumweka wakfu hapo tarehe 6 Januari 1979, kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Hayati Kardinali Macharski alikuwa ni kati ya wasomi waliotingisha Poland wakati wake. Papa Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Kardinali tarehe 30 Juni 1979. Baada ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu Jimbo kuu la Cracovia, tarehe 3 Juni 2005 akang’atuka kutoka madarakani. Kutokana na kifo cha Kardinali Franciszek Macharski, takwimu zinaonesha kwamba Baraza la Makardinali kwa sasa lina wajumbe 211 kati yao wenye sifa ya kupiga na kupigiwa kura ni 112 na wengine 99 hawana tena sifa na kupiga wala kupigiwa kura wakati wa mchakato wa kumchagua Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.