2016-08-02 15:35:00

Wananchi wanataka: Ajira, Chakula na Malazi!


Familia ya Mungu nchini Argentina tarehe 7 Agosti 2016 inaadhimisha kumbu kumbu ya Mtakatifu Gaetano msimamizi wa taifa la Argentina. Hii ni siku maalum ambayo waamini wanaonesha ibada ya pekee kwa Mtakatifu Gaetano. Baba Mtakatifu Francisko wakati akiwa Askofu mkuu wa Buenos Aires alikuwa anaitumia siku hii kwa ajili ya kuzungumza na kuwafariji waamini wake pamoja na kuwabariki watoto kwani hawa ni tumaini la Kanisa la Jamii katika ujumla wake. 

Hii ilikuwa ni siku ya sala na ibada, tukio ambalo liliwakutanisha watu kutoka sehemu mbali mbali za Argentina kwa ajili ya kumshukuru Mungu kwa mafanikio mbali mbali ya maisha, lakini ilikuwa ni siku maalum ya kumwomba Mtakatifu Gaetano awaombee riziki yao ya kila siku pamoja na kupata fursa za ajira. Hata katika mazingira kama haya, watu wanaonesha imani na matumaini kwa Mwenyezi Mungu chemchemi ya huruma na wema wote katika maisha ya binadamu.

Wazazi walikuwa wanapita huku machozi yakiwabubujika utadhani bomba la maji limekatika kutokana na uchungu wa kukosa fursa za ajira, hali inayowanyika wazazi kuweza kutekeleza vyema mahitaji msingi ya familia zao! Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Askofu mkuu Josè Maria Arancedo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina anasema, anakumbuka maadhimisho haya kwa heshima  kubwa kwani ilikuwa ni siku ya mshikamano wa kitaifa.

Watu wanatafuta riziki yao ya kila siku, ingawa ni rahisi kuweza kuipata kutokana na mshikamano wa dhati miongoni mwa waamini pamoja na taasisi za huduma ya upendo. Lakini fursa ya ajira si jambo rahisi sana kupatikana, hasa kutokana na myumbo wa uchumi kimataifa uliopelekea idadi kubwa ya watu kukosa fursa za ajira. Baba Mtakatifu anasema, kuna tofauti kubwa ya kupewa chakula na kukipeleka nyumbani kwa ajili ya kukidhi mahitaji ya familia na kuwa na chakula nyumbani kwako, kazi ya mikono na jasho lako mwenyewe, kielelezo makini cha utimilifu wa utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, watu wanapotafuta fursa za ajira wanataka kupata utimilifu wa utu na heshima yao kama binadamu. Katika maadhimisho ya sherehe ya Mtakatifu Gaetano, waamini wanataka kuwaomba waajiri kuhakikisha kwamba watu wanapata chakula cha kuweza kupeleka kwenye familia zao. Lengo ni kuweza kuwa na chakula, ajira na makazi; mambo muhimu sana katika ustawi na maendeleo ya binadamu: kiroho na kimwili na kwamba, huu ni msingi wa haki za binadamu.

Kazi inamkirimia mtu heshima na utu wake na kwa kawaida watu hawapendi kuwa ni tegemezi kwa jirani zao. Jamii ya Argentina inawaangalia watu wasiokuwa na fursa ya ajira kwa jicho la kengeza, kwani ndani mwao wanaona kuwa wanakosa utu na heshima yao kama binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anawataka Maaskofu wenzake, wajitahidi kuwaongoza na kuwasindikiza waamini wao wanaotafuta fursa za ajira na riziki yao ya kila siku. Watekeleze dhamana hii kwa moyo wa huruma na mapendo; kwa uwepo wao wa karibu na sala pamoja na kujiombea wao wenyewe fursa ya kazi inayowapatia utu na heshima yao kama binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha ujumbe wake, kwa kuiomba familia ya Mungu nchini Argentina kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala na sadaka zao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.