2016-08-02 16:17:00

Vijana sasa wanahamasishwa kuwa ni wajenzi wa amani duniani!


Kardinali Stanislaw Dziwisz, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cracovia aliyekuwa mwenyeji wa Maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani kwa mwaka 2016 katika mahojiano maalum na Radio Vatican anapenda kumshukuru Mwenyezi Mungu, Baba Mtakatifu Francisko pamoja na vijana wote walioshiriki katika maadhimisho haya ambayo yamekuwa na mafanikio makubwa katika maisha na utume wa Kanisa nchini Poland.

Vijana wamejibu kwa ari na moyo mkuu mwaliko wa Baba Mtakatifu katika maadhimisho haya; wamefurahishwa na kushangazwa na ukarimu wa pekee ulioneshwa na familia ya Mungu kutoka Poland. Vijana wamewashangaza walimwengu kwa moyo wa sala na ibada; sherehe na upendo wao kwa Baba Mtakatifu Francisko. Licha ya umati mkubwa wa vijana kiasi hiki, hakuna tukio la kusikitisha lililojitokeza. Vyombo vya ulinzi na usalama vimetekeleza dhamana na wajibu wake barabara kiasi kwamba vinastahili pongezi kubwa.

Poland imeonesha kuwa ni nchi ya amani na utulivu kwa wale wote wanaotaka kutembelea na kujizamisha kwenye chemchemi ya huruma ya Mungu! Kwani hapa ndipo mahali pake haswa! Hapa Baba Mtakatifu Francisko amewataka vijana kuwa ni vyombo, mashuhuda na mitume wa huruma ya Mungu kwa walimwengu kwa kujikita katika misingi ya haki, amani, upendo, mshikamano na udugu; daima wakiiga mifano ya waasisi wa huruma ya Mungu, yaani Mtakatifu Yohane Paulo II na Sr. Faustina Kowalska. Maadhimisho ya Jubilei ya huruma ya Mungu kwa vijana ni tukio ambalo limeacha chapa ya kudumu katika akili na nyoyo za familia ya Mungu nchini Poland.

Ni matumaini ya Kanisa nchini Poland kwamba, vijana wataweza kumwilisha changamoto na ujumbe walioupokea wakati wa maadhimisho haya kwa njia ya katekesi, hotuba na mahubiri pamoja na shuhuda mbali mbali zilizotolewa. Vijana waendelee kutoa kipaumbele kwa Mungu katika maisha yao. Kanisa linatumaini kwamba, Poland itapyaishwa baada ya maadhimisho haya kwa kujikita zaidi katika umoja na matumaini, ili kuwa na leo na kesho iliyo bora zaidi katika maisha ya kiroho, kiutu na kimaadili! Siku ya Vijana Duniani itazaa matunda kwa wakati wake!

Kwa upande wake, Kardinali Louis AntonioTagle, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa, Caritas Internationalis anasema, maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani daima ni fursa ya neema ya Mungu inayoliwezesha Kanisa kuona ubinadamu unaofumbatwa katika nyuso za vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, wakiwa tayari kupenda na kuhudumia. Hawa ni vijana wanaosukumwa na imani, matumaini na mapendo kwa Kristo na Kanisa lake na kwa mwaka huu wamehamasishwa kuwa ni vyombo, mashuhuda na mitume wa huruma ya Mungu inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu!

Kanisa na walimwengu wanayo mambo mengi ya kujifunza kutoka kwa vijana hasa wale wanaotoka katika familia maskini, vijana wanaopambana na changamoto za maisha bila ya kukata tamaa; vijana ambao wako tayari kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Caritas Poland imetoa zawadi ya nyumba mbili kwa ajili ya wazee na familia maskini kama kumbu kumbu ya matendo ya huruma wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Caritas inaendelea kujipanga ili kuboresha huduma ya afya kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji kutoka Syria wanaohudumiwa huko Lebanon. Ni matumaini ya Kardinali Louis Antonio Tagle, vijana wataendelea kuimarishwa katika imani, matumaini na mapendo, tayari kuwa ni vyombo, mashuhuda na mitume wa huruma ya Mungu kwa ndugu na jirani zao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya RadioVatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.