2016-08-01 15:31:00

Vijana wafundwe tunu msingi za ndoa na familia!


Askofu Salutaris Melchior Libena wa Jimbo Katoliki Ifakara, Tanzania katika mahojiano maalum na Radio Vatican anabainisha kwamba, Mababa wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM  katika mkutano wao 17 huko Luanda, Angola, kuanzia tarehe 18- 25 Julai 2016 ulioongozwa na kauli mbiu “familia Barani Afrika: Jana, Leo na Kesho kadiri ya mwanga wa Injili wamekazia kwa namna ya pekee majiundo makini kwa vijana na wanandoa watarajiwa! Lengo na kudumisha Injili ya Familia kadiri ya tunu msingi za maisha ya Kikristo na Kiafrika!

Mababa wa SECAM wamesisitizia uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia, mambo msingi ambayo vijana wa kizazi kipya wanapaswa kurithishwa kwa njia ya katekesi makini na endelevu. Vijana wanapaswa kuelewa dhana ya familia mintarafu Mafundisho  tanzu ya Kanisa; umuhimu wa maisha ya ndoa na familia kadiri ya mpango wa Mungu kwa mwanadamu.

Kutokana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia sanjari na ukanimungu, vijana hawana budi kupewa malezi bora na endelevu kuhusu tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni, ili waweze kusimama kidete: kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya familia. Vijana wafundwe namna ya kumtafuta, kumtumikia na kumwogopa Mungu katika maisha yao, kwani mwelekeo wa sasa ni kutaka kumng’oa Mwenyezi katika maisha na vipaumbele vya mwanadamu kwa kusahau kwamba, bila Mungu mwanadamu atajichumia majanga na kukosa amani, furaha na utulivu wa ndani!

Vijana wasaidiana kumrudisha Mungu katika maisha yao kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko; kwa kutumia mitandao ya kijamii, ili Kristo Yesu aweze kuwa kweli ni dira na nguzo ya maisha yao! Vijana wakiyaelewa mafundisho tanzu ya Kanisa kuhusu ndoa na familia, wataweza kuyatetea na kuyamwilisha, kinyume cha mwelekeo potofu kuhusu ndoa na familia.

Askofu Libena anakaza kusema, majiundo makini kuhusu ndoa na familia yanapaswa kutolewa kwa Majandokasisi wanaojiandaa kwa ajili ya maisha, wito na utume wa Kipadre, ili waweze kuwasaidia wanandoa katika safari ya maisha yao: wakati wa raha na shida na hasa wanapokumbana na changamoto kali za maisha ya ndoa na familia. Vijana watambue kwamba, ndoa kadiri ya mpango wa Mungu ni ya mume mmoja na mke mmoja na wala si vinginevyo! Vijana wasikubali kutumbukizwa katika utamaduni wa kifo! Mapadre waliofundwa barabara wanaweza kuwaimarisha waamini katika maisha ya ndoa na familia, kiasi cha kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wao wa kuzaa na kuongezeka bila kusahau kutoa malezi makini kwa watoto wao. Utume wa familia sasa unapaswa kuvaliwa njuga, ili kupambana na mielekeo potofu. Lengo ni kutangaza na kushuhudia Injili ya familia Barani Afrika!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.