2016-08-01 11:18:00

Vijana ni jeuri ya Kanisa!


Askofu Damian Muskus, Mratibu mkuu wa Maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana nchini Poland, Jumapili, tarehe 31 Julai 2016 aliwatambulisha vijana waliojitolea wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana kuwa kweli ni majembe na mashuhuda wa huruma ya Mungu, waliojisadaka usiku na mchana kwa ajili ya huduma makini kwa vijana mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Hawa ni vijana wanaopenda na kuhudumia; wanaompenda na kumwona Yesu kati ya jirani na ndugu zao wanaoteseka na kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Vijana wa kujitolea wameonja na kuonjeshana huruma ya Mungu na wanapania kuhudumia, kama sehemu ya mchakato wa majiundo yao kama mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa walimwengu; Mungu anayewataka kushuhudia upendo kwa kutambua kwamba, vijana ni matumaini ya Kanisa na Jamii kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Bikira Maria wa Kalwaria Zebrzydowska ndiye aliyekuwa Mama na mwalimu wa Mtakatifu Yohane Paulo II. Hapa ni mahali ambapo alitembelea wakati wa ujana wake, kama Padre na Askofu. Akamkabidhi matatizo na matumaini ya Kanisa. Hapa ni mahali ambapo pia vijana na mahujaji kutoka sehemu mbali mbali za dunia wametembelea ili kujiaminisha kwa Bikira Maria na hatimaye, kumkaribisha katika Sherehe ya imani miongoni mwa vijana wa kizazi kipya, kwani Kanisa linahitaji ulinzi na tunza yake ya kimama. Kanisa linawashukuru na kuwapongeza vijana waliojisadaka kwa ajili ya huduma wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016. Bila shaka wataendelea kuboresha wema na huduma yao, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.