2016-08-01 14:46:00

Papa Francisko amkabidhi B. Maria matunda ya Siku ya Vijana Duniani!


Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 31 Julai 2016 majira ya saa 3: 30 Usiku kwa saa za Ulaya aliwasili kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa “Leonardo da Vinci” mjini Roma, baada ya kuhitimisha hija yake ya kichungaji nchini Poland, kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016. Kabla ya kuelekea mjini Vatican, Baba Mtakatifu Francisko alikwenda moja kwa moja kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, mjini Roma ili kutoa heshima zake kwa Bikira Maria Afya ya Warumi kwa kuifanikisha hija yake ya kitume nchini Poland pamoja na kuyakabidhi matunda ya maadhimisho haya chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria.

Baba Mtakatifu Francisko kabla ya kuondoka, aliwaaga vijana waliokuwa wamekusanyika kwa wingi mbele ya Makao makuu ya Jimbo kuu la Cracovia kumtakia heri na safari njema. Baba Mtakatifu amewashukuru kwa wema, ukarimu na mapokezi makubwa waliyomwonesha wakati wote wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016. Baba Mtakatifu aliwapatia baraka zake za kitume na kuwaomba waendelee kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa njia ya sala na sadaka yao! Mwishoni akawambia “Do Widzenia”. Kwaheri ya kuonana!

Na padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.