2016-08-01 14:09:00

Papa achonga na waandishi wa habari na kueleza jinsi alivyoanguka!


Baba Mtakatifu Francisko wakati akirejea kutoka Poland kwenye maadhimisho ya Siku ya XXXI Vijana Duniani kwa Mwaka 2016, Jumapili tarehe 31 Julai 2016 amepata nafasi ya kuzungumza na waandishi wa habari waliokuwa kwenye msafara wake. Amemshukuru kwa namna ya pekee Padre Federico Lombardi ambaye ameitumikia Radio Vatican kwa nyadhifa mbali mbali katika kipindi cha miaka 25 na miaka 10 kama msemaji mkuu wa Vatican. Ametoa salam za rambi rambi kwa wandishi wa habari kutokana na msiba wa Anna Maria Bianchini.

Baba Mtakatifu anaishukuru na kuipongeza familia ya Mungu nchini Poland kwa wema na ukarimu wake kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Ameona ari na mwamko wa wananchi wa Poland; upendo na ukarimu wao, licha ya mvua kubwa iliyokuwa inanyeesha lakini bado walijipanga barabarani kumsalimia na kumtakia safari njema. Tangu akiwa mdogo, Baba Mtakatifu anasema, alibahatika kukutana na kuwafahamu wananchi kutoka Poland.

Baba Mtakatifu anasema, vijana ni matumaini ya Kanisa na Jamii, kumbe kuna haja ya kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi; majadiliano na “vijana wa zamani” ili kuchota urithi wa utajiri wa hekima na busara zao tayari kupambana na changamoto za maisha kwa mwanga na mwamko mpya. Watu wa makamo wanapaswa pia kujifunza kutoka kwa vijana ili kuwasaidia kukua na kukomaa katika maadili na utu wema, ili kujenga historia na kuondokana na tabia ya vijana kujifungia katika ubinafsi.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, anaendelea kutafakari kwa kina na kujadiliana na viongozi wengine kuhusu machafuko ya kisiasa nchini Uturuki. Lakini pale inapobidi, ukweli lazima usemwe na pale aliposema ukweli kuhusu Uturuki alishambuliwa kwa maneno makali. Kuhusu shutuma zinazotolewa dhidi ya Kardinali George Pell, Katibu mkuu wa Sekretarieti ya uchumi mjini Vatican bado zina utata na mashaka na katika hali kama hii kanuni maadili inasema ni kukaa kimya bila kutenda “In dubio pro reo”. Kumhukumu Kardinali Pell kwa njia za vyombo vya habari ni kutokumtendea haki.

Baba Mtakatifu Francisko anasema alianguka wakati wa Ibada ya Misa kwa sababu wakati alipokuwa akifukuzia ubani macho yake yalijikita kwenye sanamu ya Bikira Maria na kusahau kwamba, kulikuwa na ngazi, alipojisikia kwamba, alikuwa anaanguka, akajiachia bila kipingamizi vinginevyo hali ingekuwa mbaya, lakini hali yake ni nzuri. Vatican bado inaonesha utashi wa kuendeleza mchakato wa majadiliano na Serikali ya Venezuela ili kupata ufumbuzi wa amani, lakini hadi sasa hana uhakika wa ushiriki wa Vatican katika majadiliano haya ya amani.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, mauaji yanafanywa na waamini wa dini zote si tu Waislam hata Wakristo wamo ingawa hawavumi, daima katika kila dini kuna waamini wenye misimamo mikali ya kiimani wanaoshiriki katika mauaji, dhuluma na nyanyaso kwa watu wengine. Lakini kuna mauaji mengine yanayofanywa kwa njia ya ulimi ambao ni mkali kuliko hata upanga. Majadiliano ya kidini ni muhimu sana  katika kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na maridhiano kati ya watu.

Kuna waamini wa dini ya Kiislam wanaoshiriki kikamilifu katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Hii inaonesha kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa waamini wa dini mbali mbali kuishi kwa amani na utulivu licha ya tofauti zao za kidini. Utupu wa maisha ya kiutu na kiroho, ukosefu wa fursa za ajira; matumizi haramu ya dawaza kulevya na ulevi wa kupindukia ni kati ya mambo yanayochochea misimamo mikali ya kidini. Vitendo vya kigaidi vimezagaa kwa mifumo mingi kama vile mashambulizi ya kikabila hii ni kutokana na ukweli kwamba, fedha imepewa kipaumbele cha kwanza kuliko hata utu na heshima ya binadamu, kumbe vitendo vya kigaidi ni kinyume kabisa cha utu wa binadamu.

Baba Mtakatifu Francisko amechukua nafasi hii kuwasalimia na wamini wa Panama kwa kuwatakia heri na mafanikio mema katika maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019. Mwishoni, Baba Mtakatifu amemshukuru na kumpongeza Padre Federico Lombardi kwa sadaka na majitoleo yake, lakini amewakumbusha kwamba, Lombardi kwanza kabisa ni Padre na Myesuiti. Mwezi Septemba ataagwa rasmi ili kuweza kuanza utume mpya. Baba Mtakatifu amewatakia wote siku kuu njema ya Mtakatifu Inyasi wa Loyola, inayoadhimishwa kila mwaka ifikapo tarehe 31 Julai.

Na padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.