2016-08-01 12:05:00

Ama kwa hakika vijana wamewasha moto wa Injili ya huruma!


Padre Federico Lombardi baada ya kulitumikia Kanisa kwa muda wa miaka kumi kama Msemaji mkuu wa Vatican, kuanzia tarehe 1 Agosti 2016 ameng’atuka madarakani, lakini amehitimisha utume wake kwa tukio kubwa la maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 huko Cracovia, Poland lililokuwa linaongozwa na kauli mbiu “Heri wenye rehema maana hao watapata rehema”. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kwa Mwaka 2019 yatafanyika nchini Panama kama alivyotangaza Baba Mtakatifu Francisko wakati wa kufunga maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Poland, Jumapili tarehe 31 Julai 2016.

Padre Lombardi katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Poland imekuwa na mafanikio makubwa hasa kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Baba Mtakatifu amejibu kiu ya maswali na udadisi wa vijana wa kizazi kipya. Amewapatia ujumbe wa imani, matumaini na mapendo, mambo msingi kwa vijana wa kizazi hiki cha “dot com”. Vijana wanapaswa kuwa na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Baba Mtakatifu nchini Poland amefunga rasmi Jubilei ya miaka 1050 ya Ukristo nchini Poland. Amefanikiwa kukutana na kuonja imani na ukarimu wa familia ya Mungu nchini Poland. Ametembelea kambi za mateso na mauaji ya kinyama, changamoto kwa walimwengu kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Padre Lombardi anasema, familia ya Mungu nchini Poland bado ina kumbu kumbu endelevu ya Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wa Kanisa. Wamempokea Baba Mtakatifu Francisko kwa mikono miwili. Baba Mtakatifu amehitimisha hija yake ya kitume nchini Poland kwa kukutana na kuzungumza na vijana waliokuwa wanahudumia wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Amewataka kuzingatia: Kumbu kumbu ya historia yao; kuwa na ujasiri katika maamuzi yao na matumaini kwa kesho iliyo bora zaidi! Padre Federico Lombardi anasema, huu pia ni wosia kwa vijana wote walioshiriki katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.