2016-07-31 15:32:00

Ushuhuda wa changamoto za maisha ya ujana!


Mkesha wa kufunga maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani, Jumamosi, tarehe 30 Julai 2016 ulipambwa kwa shuhuda kutoka kwa vijana watatu pamoja na sanaa ya maonesho iliyogusa vituo vitano vya maisha ya ujana. Kituo cha kwanza kilionesha vijana wenye mashaka katika imani; vijana ambao wamemezwa na malimwengu na maisha ya anasa za mpito. Kituo cha pili kimewaonesha watu waliokata tamaa ya maisha kutokana na vita, dhuluma na nyanyaso.

Hiki ni kilio cha damu ya watu wasiokuwa na hatia, lakini kwa bahati mbaya hakuna anayewasikiliza kama ilivyo huko Syria na Mashariki ya Kati. Kituo cha tatu kimeonesha upendo kwa wale wasiopendeka; changamoto kwa vijana kutoka katika ubinafsi kwa kudhani kwamba, mitandao ya kijamii na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ndio utimilifu wa maisha kiasi cha kusahau kushikamana na wengine!

Kituo cha nne kimeonesha upatanisho na msamaha wa kweli ulioneshwa na kushuhudiwa na Mtakatifu Yohane Paulo II katika maisha na utume wake. Na kituo cha tano kimewaonesha vijana kwamba, Kristo Yesu ni chemchemi ya furaha, amani na utulivu wao. Matumizi haramu ya dawa za kulevya, utumwa mamboleo ni mambo ambayo yanawasababishia vijana msongo wa mawazo, upweke hasi na hatimaye kukata tamaa ya maisha na huo ni mwanzo wa kumezwa na utamaduni wa kifo!

Vijana wamesikiliza shuhuda iliyotolewa na kijana mwenzao kutoka Poland aliyemezwa na malimwengu, lakini siku moja, akaonja huruma ya Mungu katika maisha yake kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho na tangu wakati huo, amekuwa mtu mpya na ameshiriki kikamilifu katika maandalizi na maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 ili kuwasaidia vijana wa kizazi kipya kuonja furaha ya huruma ya Mungu inayomletea mwamini upya wa maisha kwa kuondolewa dhambi zao, ili kupatanishwa na Mungu pamoja na jirani zao.

Ushuhuda uliotolewa na Rand Mittri kutoka Syria uliwaacha vijana wengi wakiwa na maswali kuhusu utamaduni wa kifo, dhuluma na nyanyaso kiasi kwamba, kila siku wananchi wengi wa Syria hawana uhakika wa usalama wa maisha yao. Watu wanaendelea kupoteza maisha kutokana na vita kiasi kwamba, hata hawana tena machozi ya kuwalilia ndugu na jamaa zao! Kilio chao hakina mtu wa kuwasikiliza, lakini wanafarijika kwa njia ya ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Hata katika hali ngumu ya maisha, bado baadhi ya vijana wanaweza kuwashirikisha jirani zao huduma ya upendo na ukarimu wa maisha.

Ushuhuda wa kijana Miguel kutoka Paraguay unaonesha mapambano dhidi ya upweke hasi, matumizi haramu ya dawa za kulevya, vitendo vya kihalifu vinavyochafua kurasa na ndoto za maisha ya vijana wengi duniani na matokeo yake ni kulia na kusaga meno. Lakini vijana wa namna ya hii, wakipiga moyo konde, wanaweza kusimama tena na kuanza kuandika kurasa za maisha yao kwa wema na utakatifu wa maisha, leo hii Miguel ni kijana tofauti kabisa na jinsi alivyokuwa kwani kwake familia haikuwa ni mali kitu, nyumbani kwao palikuwa ni mahali pa kula na kulala, kiasi kwamba, hakuonja upendo na thamani kutoka kwa wazazi wake.

Kwa njia ya Neno la huduma makini cha shughuli za kichungaji kwa vijana, aliweza kuona mwanga mpya katika maisha! Anashuhudia jinsi neema, upendo na huruma ya Mungu inavyoleta mabadiliko katika maisha ya watu! Leo hii anawajibika kikamilifu na amekuwa ni mfano bora kwa vijana wenzake katika mapambano ya maisha ya kiroho dhidi ya matumizi haramu ya dawa za kulevya! Amepewa dhamana ya kuongoza kituo cha vijana wanaotaka kuachana na matumizi haramu ya dawa za kulevya huko AsunciĆ²n, Paraguay.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.