2016-07-31 14:20:00

Huruma ya Mungu ni kiini cha Injili na Ukristo!


Kardinali Stanislaw Rylko, Rais wa Baraza la Kipapa la walei baada ya maadhimisho ya Misa takatifu kufunga rasmi maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 kwenye Uwanja wa Huruma ya Mungu, Jimbo kuu la Cracovia, Jumapili, tarehe 31 Julai 2016 amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko, kwa kuwawezesha vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia kushuhudia ujana wa Kanisa na ari ya kimissionari sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ambayo yameongozwa na kauli mbiu “Heri wenye rehema maana hao watapata rehema”.

Cracovia ni mahali ambapo kuna Madhabahu ya Huruma ya Mungu; mahali walipozaliwa Watakatifu Yohane Paulo II na Sr. Faustina Kowalska, walioasisi na kuwaongoza vijana kukimbilia katika chemchemi ya huruma ya Mungu katika maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Vijana wamegundua kwamba, huruma ya Mungu ni kiini cha Injili na Ukristo; kwani Ukristo na huruma ya Mungu ni sawa na chanda na pete!

Yesu mwingi wa huruma na mapendo, ameonesha jicho lake kwa vijana, kiasi cha kujifanyia maamuzi muhimu katika maisha na miito mbali mbali yaani: Ndoa, Upadre na Utawa. Vijana wameonja furaha, umoja, udugu na mshikamano pamoja na kushuhudia kwamba, inapenda na kulipa kuwa Mkristo na kumfuasa Kristo pasi na makunyazi moyoni! Baada ya maadhimisho haya vijana wanapenda kumshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu kwa kushiriki kikamilifu katika maadhimisho haya, lakini hasa kwa neno na changamoto za maisha; kwa matumaini na ujasiri unaopaswa kushuhudiwa na vijana duniani! Mwisho wa maadhimisho haya ni mwanzo wa utekelezaji wa ari na mwamko wa umissionari kwa vijana kuwa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu, tayari kuwasha moto wa huruma, ili kudumisha amani na furaha. Vijana wanaporejea makwao, wawe kweli ni mitume na mashuhuda wa huruma ya Mungu.

Kwa upande wake, Kardinali Stanislaw Dziwish, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cracovia anasema, vijana wataendelea kuimba utenzi wa huruma ya Mungu pasi na mwisho. Vijana wamekuwa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya furaha; ari na mwamko wa imani na matumaini katika ulimwengu ambamo ubaya unaonekana kana kwamba, unatawala kwa kusababisha: vifo, mateso na mahangaiko kwa watu. Lakini matumaini ni dira na njia inayofumbata upendo na huduma inayojielekeza katika maisha.

Familia ya Mungu nchini Poland inamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu kwa uwepo, ushiriki, maneno na faraja yake; mambo ambayo yanaonesha Ubaba wake. Vijana wanahamasishwa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa matumaini na huruma ya Mungu. Anawashukuru wote waliosaidia kufanikisha maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 huko Cracovia, nchini Poland. Hili ni tukio la imani, matumaini na mapendo, ambalo litaacha alama ya kudumu katika maisha ya Kanisa na Ulimwengu katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.