2016-07-31 15:14:00

Hakuna lugha nyingine tena isipokuwa imani, udugu na upendo!


Kardinali Stanislaw Dziwicz wakati akimkaribisha Baba Mtakatifu Francisko pamoja na vijana katika mkesha wa kufunga maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani, Jumamosi, tarehe 30 Julai 2016 amesema, haya yalikuwa ni maandalizi kwa ajili ya kuhitimisha sherehe ya imani kwa vijana kwa mwaka 2016. Hawa ni vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia waliokusanyika kwenye Uwanja wa huruma ya Mungu ili kumzunguka Kristo Yesu.

Ni vijana ambao kimsingi wanazungumza lugha mbali mbali kutokana na tamaduni zao, lakini wakati wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa pamoja wamezungumza lugha ya imani, udugu na upendo. Vijana walikuwa tayari kusikiliza kwa makini ujumbe kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, anayewashirikisha lugha ya upendo. Taarifa zinaonesha kwamba, katika mkesha huu, walikuwepo vijana zaidi ya millioni moja laki sita, lakini pia kulikuwa na umati mkubwa wa vijana wa kizazi kipya pamoja na vijana wa zamani waliounganika kushuhudia tukio hili kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya jamii.

Watu wote hawa wamesalimiwa kutoka Cracovia, mahali walipozaliwa watakatifu Yohane Paulo II na Sr. Faustina Kowalska, waasisi wa Ibada ya huruma ya Mungu ambayo kwa sasa imeenea sehemu mbali mbali za dunia! Kardinali Dziwicz anasema, vijana ni tumaini la Kanisa na Ulimwengu katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo. Hawa ndio wahusika wakuu watakaotekeleza mustakabali wa mataifa, jumuiya na familia zao. Hawa ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya amani, kwa umakini na matumaini. Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani yamewasaidia kuwafunda ili kutekeleza dhamana hii kwa siku za usoni.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.