2016-07-30 10:54:00

Endeleeni kuandika Injili ya Kristo kwa matendo ya huruma!


Baba Mtakatifu Francisko ameianza Siku ya Jumamosi tarehe 30 Julai 2016 kwa kutembelea Madhabahu ya Huruma ya Mungu; baadaye akatembelea pia Kikanisa cha Mtakatifu Sr. Faustina Elena Kowalska (1905- 1938). Hapo Baba Mtakatifu alipata nafasi ya kusali kwa kitambo kidogo mbele ya kaburi la Mtakatifu Faustina na baadaye akaweka sahihi kwenye kitabu cha wageni mashuhuri. Baba Mtakatifu amewasalimia vijana waliokuwa kwenye uwanda wa maungamo kati ya Madhabahu ya huruma ya Mungu na Madhabahu ya Mtakatifu Yohane Paulo II pamoja na kukutana na watoto wagonjwa.

Baba Mtakatifu amepitia katika Lango la Huruma ya Mungu kwenye Madhabahu ya Huruma ya Mungu na baadaye akashiriki katika kuwaungamisha vijana watano. Amepata nafasi pia ya kusali kwa kitambo kirefu mbele ya Ekaristi Takatifu. Majira ya saa 4: 15 akaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Wakleri na Watawa kutoka Poland. Katika mahubiri yake, Baba Mtakatifu Francisko amekazia kwa namna ya pekee umuhimu wa mahali, mtume na kitabu ambacho kinapaswa kuandikwa kila siku kwa matendo ya huruma!

Siku ile ya Pasaka anasema Baba Mtakatifu wanafunzi wa Yesu walikuwa wamejifungia ndani kwa hofu ya kipigo cha Wayahudi. Yesu akatokeza kati yao na kuwakirimia amani na Roho Mtakatifu, ili waweze kuwaondolewa watu dhambi zao yaani kuwagawia watu huruma ya Mungu. Hapa Yesu aliwatuma wafuasi wake kwenda duniani, ili kuitangaza na kuishuhudia huruma ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia, kama alivyofanya mwenyewe katika hali ya unyenyekevu na utumishi bila majigambo!

Wafuasi wa Yesu wanatumwa kutangaza Habari Njema ya Wokovu inayowakirimia watu msamaha, amani na nguvu ya Roho Mtakatifu. Waamini wanaalikwa kwa namna ya pekee na Mtakatifu Yohane Paulo II kumfungulia Kristo malango ya maisha yao, lakini kishawishi cha Wakleri na Watawa kutaka kuendelea kujifungia katika undani wao ni kikubwa sana, lakini Yesu anawataka kutoka huko walikojificha, ili kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake bila ya kujibakiza hata kidogo bali kwa kujiaminisha na kuandamana na Kristo peke yake katika maisha.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, viongozi wa Kanisa kwa namna ya pekee, wanaalikwa kumwilisha upendo katika huduma kwa kuwajibika barabara na kwenda mahali ambapo watu wana kiu ya huruma na upendo wa Mungu. Hii ni huduma kwa ajili ya Kanisa zima, mahali ambapo Wakleri na Watawa wanaweza kutekeleza dhamana na utume wao bila ya kujibakiza au kutafuta mafao yao binafsi! Hii ni dhamana ya Uinjilishaji mpya unaojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kinyume kabisa cha ubinafsi, ukosefu wa matumaini na furaha. Viongozi wa Kanisa wawe na ari ya kumshuhudia Kristo kwa kuthubutu kuendelea kuwa waaminifu kwa dira na mwongozo unaotolewa na Roho Mtakatifu, ili kuinjilisha kwa kina!

Baba Mtakatifu anasema, Injili inamwonesha Mtakatifu Toma, Mtume, mtu mwenye mashaka anayependa kugusa ili aweze kuamini na Yesu Kristo anamshangaza Toma kwa kumwonesha na kumgusisha Madonda yake matakatifu, alama ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Wafuasi wa Kristo wanapaswa kushikamana na Kristo Yesu katika ukweli, imani na matumaini, kwani anayafahamu maisha na siku za kila mmoja wao.

Wafuasi wa Kristo wawe na ujasiri wa kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu kuhusiana na mapungufu yao ya kibinadamu, mchoko na hata ukakasi wa maisha. Moyo Mtakatifu wa Yesu unawafumbata wale watu ambao ni wa kweli, watu wanaoweza kusikitika kutokana na mapungufu yao ya maisha, lakini wakiwa na imani katika huruma ya Mungu. Yesu anaitafuta nyoyo ambayo inaonesha unyenyekevu na wala si ile migumu kama jiwe! Anataka nyoyo zinazoonesha toba tayari kumwilisha msamaha na huruma ya Mungu kwa jirani zao.

Mfuasi wa Yesu anapokuwa katika mashaka hawezi kusita kuwashirikisha viongozi wake! Mfuasi mwaminifu anafanya mara kwa mara mang’amuzi ya maisha yake kwa kutambua kwamba moyo wa mwanadamu hauna budi kufundwa kila siku ili kuondokana na unafiki katika maisha! Baada ya mahangaiko makubwa hatimaye, Mtakatifu Toma, Mtume aliweza kuamini katika Fumbo la Pasaka na kumwambata Kristo Yesu katika maisha yake yote, kwa kutambua kwamba, Kristo ni kilele cha wema wake wote, njia katika maisha yake, moyo wa maisha na kila kitu alicho nacho! Hii ni sala ambayo viongozi wa Kanisa wanaweza kuisali kila siku!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Injili ni kitabu ambacho maisha na matendo makuu ya Yesu yameandikwa ndani mwake, changamoto na mwaliko kwa waamini  kutangaza na kushuhudia huruma ya Mungu katika maisha yao. Injili ni kitabu hai cha huruma ya Mungu kinachopaswa kusomwa na kuandikwa upya kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Bikira Maria, Mama wa huruma ya Mungu awasaidie waamini kuona Madonda matakatifu ya Yesu kwa jirani zao, tayari kuandika Injili ya huruma ya Mungu kwa njia ya huduma makini kwa maskini na wagonjwa; kwa wakimbizi na wahamiaji; daima wakitafuta kukuza na kudumisha mafao ya waamini waliokabidhiwa kwao na Mama Kanisa sanjari na kudumisha umoja wa Kanisa la Kristo! Kila mmoja wao anapaswa kutambua kwamba ndani mwake anatunza ukurasa binafsi wa kitabu cha huruma ya Mungu inayofumbatwa katika wito wao na upendo ambao ulileta mageuzi makubwa kwa kuacha yote na kuamua kumfuasa Kristo Yesu. 

Wakleri na Watawa wawe na moyo wa shukrani wanapokumbuka wito wao, waendelee kuadhimisha Fumbo la Ekaristi Takatifu, kiini cha maisha na utume wa Kanisa sanjari na kumshukuru Kristo Yesu aliyewakirimia huruma ya Mungu hata pale malango ya maisha yao yalipokuwa yamefungwa. Kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Toma, mtume, kila mtu anaitwa na Kristo kwa jina na kuendelea kuwapatia neema na nguvu ya kuandika Injili yake kwa njia ya upendo!

Mara baada ya maadhimisho ya Misa Takatifu, wawakilishi 12 wa Vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia waliweza kushiriki chakula cha mchana pamoja na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Makao makuu ya Jimbo kuu la Cracovia, nchini Poland.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.