2016-07-29 13:36:00

Vijana Poland wafunika wakati wa sherehe ya imani!


Kardinali Stanislaw Dziwisz, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cracovia akimkaribisha Baba Mtakatifu kuzungumza na bahari ya vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia, Alhamisi, tarehe 28 Julai 2016 kwenye Uwanda wa Blonia, alisema kwa sasa Poland imezama katika sherehe ya imani inayowawezesha waamini kujisikia kuwa ni sehemu ya Jumuiya ya Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu!

Hapa ni mahali ambapo aliishi Mtakatifu Yohane Paulo II, muasisi wa Siku ya Vijana Duniani, Cracovia ni mji ambao ni kisima cha huruma ya Mungu, kutokana na uwepo na ibada iliyoenezwa na Mtakatifu Faustina, mtume wa huruma ya Mungu! Kardinali Dziwisz kwa namna ya pekee, amechukua nafasi hii kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko na vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaohudhuria Siku ya XXXI ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016.

Uwepo wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ni alama muhimu sana katika kukuza na kudumisha utume wa Kanisa miongoni mwa vijana mintarafu imani ya Kanisa katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo! Maadhimisho haya pia yamehudhuriwa na watu wenye umri mkubwa, lakini wote wanajisikia kuwa na moyo wa ujana, kwani Injili daima ina mwelekeo wa ujana na upya wa maisha na inazungumza na watu wa kila rika.

Kanisa linaamini kwamba, Kristo Yesu anayo maneno ya uzima wa milele na kwamba ni Yeye peke yake anayeweza kuzima kiu ya maisha ya kiroho. Dunia ya leo amani na utulivu vinatoweka, lakini vijana wanataka kuwa ni majembe ya amani duniani; mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu, tayari kushiriki katika ujenzi wa dunia inayosimikwa katika utu na mshikamano wa dhati.

Kabla ya kuwasili kwa Baba Mtakatifu Francisko eneo hili, vijana walifanya sherehe kubwa iliyokuwa inayongozwa na changamoto ya kuwa watakatifu. Yalifuatia maandamano ya vijana waliokuwa wamebeba bendera na picha za mashuhuda wa huruma ya Mungu kutoka Ulaya: Mtakatifu Vincent wa Paulo, Barani Asia ni Mwenyeheri Mama Theresa wa Calcutta, Oceania ni Mtakatifu Maria MacKillop; Kutoka Barani Afrika ni Mtakatifu Josephine Bakhita; Amerika ya Kaskazini ni Mtakatifu Damiani De Veuster wa Molokai na Amerika ya Kusini ni Mwenyeheri Irma Dulce.

Hili ni tukio ambalo limeacha chapa ya kudumu katika nyoyo za vijana wanahudhuria maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2016 huko Cracovia, Poland.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.