2016-07-28 11:31:00

Yaliyojiri wakati wa mazungumzo ya Papa na Maaskofu wa Poland


Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 27 Julai 2016 baada ya kuzungumza na viongozi wa Serikali, wanasiasa na wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao Palond, alipata pia nafasi ya kuzungumza kwa faragha na Baraza la Maaskofu Katoliki Poland ambalo linaundwa na Majimbo 45 na kuongozwa na Maaskofu 211. Baba Mtakatifu alitumia nafasi hii kuungana na Maaskofu wote wa Poland kwa ajili ya kumkumbuka na kumwombea Marehemu Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya huduma kwa wafanyakazi katika sekta ya afya aliyefariki dunia hivi karibuni.

Maaskofu pia wamesali kwa ajili ya kumwombea Kardinali Franciszek Macharski ambaye amelazwa hospitalini mjini Cracovia. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi asubuhi baada ya kutoka kwenye Monasteri ya Kutolewa kwa Bikira Maria, alikwenda kumsalimia Kardinali Macharsi, hospitalini. Kardinali Macharsi ndiye aliyemrithi Papa Yohane Paulo II mara baada ya kuchaguliwa kwake kuliongoza Kanisa Katoliki.

Baba Mtakatifu Francisko akizungumza na Maaskofu Katoliki Poland wamegusia tema mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa. Amejibu maswali kadhaa kutoka kwa Maaskofu. Ukanimungu unavyoanza kupenyeza katika maisha ya familia ya Mungu nchini Poland na kwamba, dawa yake ni Kanisa kuwa karibu zaidi na walimwengu pamoja na kuhakikisha kwamba, wanasaidia kumwilisha tunu msingi za Kiinjili kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Kristo anapaswa kuwa karibu na watu.

Maaskofu wajenge utamaduni wa kuwa karibu zaidi na Wakleri wao kwani hawa ndio wasaidizi wao wa kwanza katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu pamoja na kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa. Vijana wanapaswa kuendelea kufundwa katika maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni kwa kushirikiana na wazee ambao wamesheheni hekima na busara ya maisha. Wazee wana uwezo wa kurithisha imani pamoja na kuhakikisha kwamba, kweli Kanisa linakuwa ni chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu: kiroho na kimwili.

Baba Mtakatifu amewaonya Maaskofu kutomezwa na malimwengu kwa kupenda mno fedha, mali na vyeo. Leo kila kitu kinawezekana kutokana na nguvu ya fedha! Lakini, Kanisa liwaendelee watu kwa: upendo na huruma na kamwe lisimezwe na malimwengu! Baba Mtakatifu anakaza kusema, Parokia bado inaendelea kuwa ni mahali muhimu sana pa ujenzi wa familia ya Mungu kwa: kusikiliza Neno, Kuadhimisha Sakramenti pamoja na kujenga mshikamano wa huruma na upendo. Parokia itaendelea kuwa ni nyumba ya watu wa Mungu.

Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu wa Poland kuongozwa na hekima na busara ya kichungaji katika kuwakirimu na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji ambao kwa sasa ni changamoto kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa. Kanisa lipime uwezo, utamaduni na fursa zilizoko ili kuwahudumia vyema wakimbizi na wahamiaji kwa kuliwezesha Kanisa kuwa wazi, ili kuonesha moyo wa upendo na ukarimu katika maeneo husika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.