2016-07-28 10:39:00

Papa asema : Dunia iko katika vita vya madaraka na siyo vita vya kidini,


(Vatican Radio) Baba Mtakatifu Francisko Jumatano akijibu hoja zilizotolewa na  kundi la wanahabari walio kuwa nae   ndani ya ndege kuelekea Krakow Poland, alirejea matendo ya kigaidi ya hivi karibuni, yakiwemo mauaji ya Padre huko Ufaransa, akisema,  dunia iko katika vita. Lakini akasisitiza kwamba , siyo vita ya dini, bali ni vita ya madaraka.

Aliweka wazi kwamba wanapozungumzia ghasia na fujo za kigaidi, katika ukweli wake ni kuzungumzia vita lakini si vita vya kidini bali vita vya kiuchumi,  maslahi, fedha, maliasili na utawala.  Na kwamba si vita vya kidini kwa kuwa dini zote zina hamu ya kuishi kwa amani.  Lakini watu wengine wanataka vita kwa maslahi yao wenyewe binafsi .

Papa Francisko alieleza na kuongeza  kwamba,  neno linalotumiwa  mara nyingi sana sasa ni "ukosefu wa usalama" lakini, akasema, neno hilo maana yake halisi ni "vita”. Dunia iko katika vita, lakini kila vita hupiganwa kwa mtindo wake kama historia inavyooneysha vita vya 1914 ilikuwa na mtindo wake, pia  vita ya 1939-1945 vilikuwa na mtindo wake na vita ya sasa ina mtindo wake. Aliongeza vita ya wakati huu,  haina sana umbile lakini ni vita ya kupangwa.

 Papa alieleza kurejea jinsi  Padre mkweli, mtu wa haki alivyo uawa wakati akitolea sala ya kuomba amani. Alimtaja Padre huyo kuwa ni mmoja tu wa wahanga wa vita hivi, kwa kuwa kuna  Wakristo wengi tu,  watu wengi wasio na hatia, watoto na watu wazima wanaouawa bila hatia kama ilivyo huko Nigeria, kwa mfano.. Alieleza na kuongeza kuwa , hakuna kuhofu kusema ukweli huu, kwamba dunia iko katika vita kwa sababu ni kweli dunia imepoteza mwelekeo wa maisha ya amani.

Na akizungumza kuhusu Mkusanyiko wa Vijana Poland kwa ajili ya Siku ya Vijana Duniani, alionyesha matumaini yake kwa vijana ambao  daima huonyesha matumaini. .Na hivyo alitumaini  katika Mkusanyiko huu wa vijana Poland,  walau utaweza  onyesha tumaini kidogo kwa dunia ya leo.

Pia Papa aliutumia muda huo kutoa shukurani zake za dhati kwa wote waliomtumia rambirambi kufuatia kuuawa kwa Padre Hamel wa Ufaransa, na hasa alitaja kufarijiwa sana na maneno ya rambirambi kutoka kwa Rais Hollande wa Ufaransa, ambaye alipiga simu na kuwa na maongezi nae kama ndugu.

Padre Federico Lombardi akiwatambulisha wanahabari kwa Papa alitaja idadi ya wanahab ari waliokuw akatika ndege hiyo kuwa zaidi ya 70 na walitoka katika nchi tofauti 15, wakiwa tayari  katika huduma ya kueneza ujumbe na maneno ya Papa, katika siku hizi muhimu za ziara yake Poland. 








All the contents on this site are copyrighted ©.