2016-07-28 09:42:00

Papa ahimiza viongozi wa Poland kuwapokea wakimbizi wa vita


(Vatican Radio) Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano akikutana na viongozi wa kisiasa nchini Poland,  alitoa wito wa kuwapokea watu wanaokimbia ghasia za vita na maafa asilia hasa yanayosababisha ukosefu wa mahitaji msingi kwa binadamu kama chakula na maji, na wakati huohuo kuhakikisha maisha ya binadamu yanalindwa tangu wakati wa kutungwa mimba hadi kifo chake cha kawaida. Papa alieleza hili, wakati akikutana na Rais wa Jamhuri ya Poland , Waziri Mkuu na viongozi wengine wa Kisiasa na wanadiplomasia waliokuwa wamekusanyika katika ukumbi wa kihistoria wa Wawel Krakow.

Hotuba ya Papa ilionyesha kuzingatia kwamba,  hii ilikuwa ni ziara yake ya kwanza katika eneo la Ulaya ya Kati Mashariki. Hivyo alilenga katika umuhimu wa historia  ya taifa hilo, iliyoweka  utambulisho wa taifa katika misingi ya rasilimali watu na kiroho, akirejea adhimisho la hivi karibuni ya  miaka 1.050 ya Mkristo wa kwanza kubatizwa Poland. Alilitaja adhimisho hili kwamba, limeweka  alama ya  nguvu ya umoja wa kitaifa na maridhiano thabiti katika njia yao ya  kufanikisha ustawi wa raia wote wa Poland,  licha ya utofauti wa maoni.

Papa pia alizungumzia  matunda ushirikiano katika nyanja za kimataifa na  kukua kwa kuheshimiana kunakotokana na utambuzi wa mtu kuheshimu utambulisho wake mwenyewe binafsi na pia kutambua utambulisho wa wengine. Alisema, hapawezi kuwa na majadiliano ya kweli, iwapo mtu mwenyewe binafsi hajui vyema utambulisho wake mwenyewe. Na kwamba katika maisha ya kila siku ya kila mtu na jamii, huwa kuna  aina mbili ya kumbukumbu: nzuri na mbaya. Alitolea mfano wa moja ya kumbukumbu nzuri katika  Biblia ni wimbo wa Mkuu wa Bikira Maria ambaye anamsifu Bwana na kazi zake kuokoa. Upande wa  kumbukumbu hasi, alitaja  jinsi moyo wa binadamu unavyomezwa na maovu, hasa makosa yaliyofanywa na watu wengine.

Aliendelea kuitazama historia ya Poland na kumshukuru Mungu, kwa kusherehekea miaka hamsini  ya sadaka ya msamaha na kuheshimiana  kati ya Mabaraza mawili ya Maaskofu, Maaskofu wa Poland na Maaskofu wa Ujerumani kwa yaliyotokea  wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.  Pamoja na azimio la pamoja kati ya Kanisa Katoliki nchini Poland na Kanisa la Orthodox la Moscow, na kitendo kilichozindua taratibu za mchakato wa kujenga  uhusiano na udugu si tu kati ya Makanisa mawili, lakini pia kati ya watu wa mataifa haya mawili.

Papa pia alizungumzia changamoto zinazokabili taifa la Poland kwa wakti huu , ikiwa ni pamoja na hali ngumu ya uchumi , masuala ya mazingira na uzushi tata wa uhamiaji. Kwayo Papa alitoa wito wa kuifungua wazi mioyo katika kukabili changamoto hizi , na hasa katika kuwa tayari kuwapokea wale wanaokimbia migogoro ya vita na wale wanaonyimwa haki zao msingi. Wakati huohuo akiomba aina mpya ya ushirikiano wa kimataifa unaoweza kuendeleza mazuri na kutatua matatizo yanayolazimisha watu kuondoka katika nchi zao za asili.  Aliongeza hili linahitaji ujasiri wa ukweli na utuzaji wa  ahadi ya kimaadili, ili kuhakikisha kwamba maamuzi na matendo, katika uhusiano wa binadamu, siku zote unaheshimu hadhi ya mtu.

Akizungumzia upande wa Kanisa alisema, Kanisa hutenda kupitia mashirika yake kama Caritas , mashirika ya Wakimbizi au huduma za Parokia na majimbo, katika  mwanga wa historia yake ya ukarimu . Bahati mbaya alisema bado kuna mamilioni ya watu ambao wanaendelea kuzikimbia nchi zao asili kwa sababu za kukosa ufumbuzi wa kisiasa na kiuchumi ikiandamana na ukosefu wa haki unaoendeleea kushuhudiwa katika dunia ya leo.

Mwisho Papa Francisko, alitoa mwaliko kwa Taifa la Poland , kuw ana matumaini kwa siku za usoni, akisema kwa mtazamo kama huo inawezekana kutengeneza mazingira mazuri ya heshima katika utendaji wote wa  jamii na pia uwepo wa mijadala ya kujenga licha ya kuwa na  maoni tofauti. Papa ameihakikisha Poland ushirikiano wa Kanisa Katoliki , ili kwamba katika mwanga wa misingi yake ya Kikristo , iliyounda historia na utambulisho wa taifa la Poland, katika hali za mabadiliko ya kihistoria , litaendelea kusonga mbele katika mapokeo ya utamaduni wake, kwa uaminifu na matumaini , hata katika nyakati ngumu . 








All the contents on this site are copyrighted ©.