2016-07-28 11:06:00

Familia ya Mungu Poland: Waaminifu kwa Mungu, Msalaba, Injili na Kanisa


Askofu mkuu Wojciech Polak wa Jimbo kuu Gniezno, Poland mara baada ya maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kama sehemu ya kilele cha Jubilei ya miaka 1050 ya Ukristo nchini Poland, Alhamisi, tarehe, 28 Julai 2016 amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuweza kuwarejesha tena katika Kisima cha Ubatizo katika ya maisha yanayoongozwa na Kristo Yesu, ufunuo wa huruma ya Mungu. Familia ya Mungu nchini Poland inataka kujiaminisha kwa Kristo na Kanisa lake, ili kuwa kweli waaminifu kwa Mungu, Msalaba, Injili na Kanisa!

Askofu mkuu Polak amekumbusha kwamba, katika maadhimisho ya Miaka 100 ya Ukristo nchini Poland, Papa Paulo VI hakuweza kuhudhuria kutokana na sababu za kisiasa, lakini aliwasindikiza kwa uwepo wake kwa njia ya sala. Kanisa nchini Poland, siku zote limeonesha kiu ya kutaka uwepo wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili aweze kuwaimarisha ndugu katika imani, matumaini na mapendo. Wanamshukuru Baba Mtakatifu kwa kuwarejesha tena katika chemchemi ya ule upendo wa kwanza na kwa njia ya mfano bora wa maisha yake wameweza kuipokea zawadi ya Jubilei ya miaka 1050 ya Ukristo sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu; matukio yote yaisaidie familia ya Mungu nchini Poland kujenga na kudumisha umoja na mshikamano lakini zaidi kwa wale wanaohitaji msaada!

Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu kwenye Madhabahu ya Jasna Gòra, imekuwa ni fursa kwa Kanisa la Poland kumzunguka Khalifa wa Mtakatifu Petro, mahali ambapo Kardinali Stefan Wyszynski na Yohane Paulo II waliweza kujiachilia chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria. Kanisa nchini Poland limemhakikishia Baba Mtakatifu Francisko kwamba, litaendelea kumsindikiza katika maisha na utume wake kwa kumweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Jasna Gòra. Familia ya Mungu ina kiu ya uwepo wa Khalifa wa Mtakatifu Petro anayewashirikisha Injili ya furaha!

Kwa upande wake Padre Arnold Chrapkowski, Mkuu wa Shirika la Wapaulini amemshukuru Baba Mtakatifu kwa kutembelea Monasteri ya Jasna Gòra, mahali ambapo kwa takribani miaka 600 Bikira Maria, Malkia wa Poland anailinda familia ya Mungu kwa uwepo na upendo wake wa kimama, kuelelekea katika utimilifu wa nyakati. Hapa ni mahali ambapo waamini wanasali bila kuchoka, ili kujichotea neema na baraka kwa ajili ya huduma kwa jirani katika umaskini na magumu ya maisha wanayokabiliana nayo. Katika maadhimisho ya Jubilei ya miaka 1050 ya Ukristo nchini Poland, wanataka kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.