2016-07-27 11:49:00

Vijana mnahamasishwa kutangaza na kushuhudia imani yenu!


Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 26 Julai anaadhimisha Kumbu kumbu ya Watakatifu Joakim na Anna, wazazi wake Bikira Maria. Hii imekuwa pia ni siku kwa ajili ya kuombea maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani kwa mwaka 2016. Itakumbukwa kwamba, kuna umati mkubwa wa vijana ambao hawakupata nafasi ya kwenda nchini Poland kuhudhuria maadhimisho haya, lakini wanashiriki kikamilifu kiroho na kimwili! Jimbo Katoliki la Brownsville, Texas, Marekani, limeadhimisha kumbu kumbu ya watakatifu Joakim na Anna sanjari na Siku ya Vijana Duniani kwa mwaka 2016.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video anawakumbusha vijana hawa kwamba, wako karibu sana na Amerika ya Kusini, wameungana pamoja kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Vijana na kwamba, anataka kuonesha ukaribu wake kwao, kwa kuwatia shime ya kusonga mbele bila kukatishwa tamaa na kuta zinazojengwa mbele yao. Vijana waoneshe ujasiri wa kupenda zaidi na kuangalia ndani mwao, urithi mkubwa ambao wamepokea kutoka kwa ndugu na jamaa. Huu ni urithi wa imani wanayopaswa kuitangaza, kuishuhudia na kupambana fika na maisha.

Baba Mtakatifu anawataka vijana kuwa ni vyombo vya huruma na mapendo sanjari na kuhakikisha kwamba, imani yao inazaa matunda ya maisha, matumaini na huruma. Vijana wawe wepesi kupokea na kugawa huruma kwa wengine; wawe pia ni chemchemi ya furaha pasi na woga. Anawatakia heri na baraka wanapoungana na vijana wenzao huko Cracovia nchini Poland kwa ajili ya kuadhimisha Siku ya XXXI ya Vijana Duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.