Waislamu, Wakristo na serikali wanapaswa kuwa macho na jaribio lolote lile linalotaka kuitumbukiza jamii katika mtego wa kutoelewana. Ni lazima Wamisri na watu wote kutambua kwamba, wale wote wanatakaobainika kuchochea au kuhusika na vurugu za kidini au mashambulizi, watakabiliwa na mashitaka na kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria kwa sababu "Misri inaongozwa kwa utawala wa sheria. Rais wa Misri Abdel Fattah al Sisi, alieleza wakati akiitoa msimamo wake, kuhusu vurugu za mapigano ya kikabila ya hivi karibuni hasa katika wilaya ya Minya, ambako ghasia hizo zilisababisha Mkristo wa Kanisa la Kikoputiki kuuawa na wapiganaji wa Kiislamu. Rais al Sisi alitoa onyo hilo wakati wa sherehe za kukabidhi vyeti wanajeshi. Katika khafla hiyo, alitoa wito wa maelewano kati ya dini na makabila, akitaja pia dhamira yake ya kumfikisha mbele ya sheria mtu yeyote anayetaka kuzua machafuko au kuanzisha vita kati dini.
Shirika la habari za Fides limetaarifu kwamba,Rais Al-Sisi alitoa wito kwa Wamisri wote kufanya kazi za kukuza umoja wa kitaifa, huku akiwahakikishia kwamba, sheria za Misri zinatambua kwamba, Wakristo na Waislamu wote ni sawa kisheria.
Nae Mkuu wa Kanisa Misri, Patriaki Tawadros II, baada ya mkutano mfupi na Rais al Sisi, aliuhutubia mkutano wa wanahabari akisisitiza pia kwamba,watu wote ni sawa na hakuna kisingizio cha watu kutaka kunufaika na matukio yanayodharirisha umoja wa kitaifa . Na kwamba, licha ya matatizo makubwa ya kiuchumi na uhaba wa rasilimali na fedha, hizo si sababu za kufanya uharifu nchini Misri.
Matamko kutoka kwa viongozi hawa wawili, Rais al Sisi na Patriaki Tawadros, yalifuatiwa pia na kauli kama hiyo kutoka kwa Sheikh Ahmed al Tayyib, al Azhar Grande Imamu, ambaye pia aliutaka umma wa Misri, kuheshimiana na kuung’oa mzizi wa fitina na vurugu kati ya makundi ya kidini.
Shirika la kujitegemea la Juhudi za Misri kwa Haki Binafsi , limetaja uwepo wa matukio zaidi 77 ya ghasia za kidini katika mkoa wa Minya tangu jaribio la 'mapinduzi ’ya Januari 26, 2011. Na kwamba, kwa wakati huu, katika matukio mengi, hatua za kisheria zimechukuliwa, kuwatambua na kuwafikisha mbele ya sheria wote wanaohusika na ghasia,hasa kupitia juhudi za mikutano ya maridhiano, inayoandaliwa na utawala mahalia , kwa lengo la kuwaweka pamoja waamini na wanachama wa jumuiya mbalimbali za kidini, kwa ajili ya ujenzi wa amani. Na wengi wameipokea kama ni njia inayofaa kuchukuliwa kukomesha vurugu na ghasia.
All the contents on this site are copyrighted ©. |