2016-07-25 10:44:00

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani: Poland kumekucha!


Baraza la Maaskofu Katoliki Poland tayari limekamilisha maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani yanayoanza kutimua vumbi rasmi hapo tarehe 27 Julai 2016 kwa uwepo mkamilifu wa Baba Mtakatifu Francisko, tayari kuwahamasisha vijana kuwasha moto wa Injili ya huruma ya Mungu kwa watu wa mataifa. Taarifa zinaonesha kwamba, tayari makundi makubwa ya vijana yanaendelea kuwasili nchini Poland pamoja na kuendelea kufanya hija kwenye maeneo maalum yatakayogusa kwa namna ya pekee maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.

Padre Federico Lombardi, Msemaji mkuu wa Vatican anafafanua kwamba, maadhimisho haya ni hija ya imani, mshikamano na upendo miongoni mwa vijana hasa wakati huu, Bara la Ulaya linapokabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo za vitisho vya vitendo vya kigaidi pamoja na mpasuko wa Jumuiya ya Ulaya ambao unaendelea kusababisha madhara makubwa hasa miongoni mwa vijana. Ulinzi na usalama unaendelea kuimarishwa nchini Poland ili kuhakikisha kwamba, maadhimisho ya Siku ya XXXI ya Vijana Duniani yanakwenda kama yalivyopangwa.

Padre Lombardi anasema, Baba Mtakatifu Francisko pamoja na vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanakwenda nchini Poland kwa imani na matumaini kwamba, maadhimisho haya yatakuwa ni sherehe kubwa ya imani na mshikamano miongoni mwa vijana kumzunguka Baba Mtakatifu Francisko. Padre Lombardi anakiri kwamba, kutokana na kuongezeka kwa wimbi la vitendo vya kigaidi Barani Ulaya, baadhi ya makundi ya vijana yameamua kutoshiriki.

Vijana wanataka kuadhimisha sherehe ya imani na mshikamano Jimboni Cracovia, mahali alipozaliwa na kutekeleza utume wake kama Askofu, Mtakatifu Yohane Paulo II, muasisi wa Siku ya Vijana Duniani, urithi mkubwa kwa maisha na utume wa Kanisa kwa vijana wa kizazi kipya. Vijana wanataka kuwasha moto wa Injili ya huruma ya Mungu kwa kushikamana na Baba Mtakatifu Francisko wakati huu, Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, changamoto na mwaliko kwa vijana kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya huruma ya Mungu. Hiki ni kielelezo na ushuhuda wa imani tendaji inayoacha chapa ya kudumu katika mchakato wa Uinjilishaji mpya.

Padre Lombardi anasema, Baba Mtakatifu atapata nafasi ya kuzungumza ana kwa ana na Baraza la Maaskofu Katoliki Poland, mazungumzo ambayo yatakuwa ni faragha bila ya kuwa na hotuba maalum iliyoandaliwa wala uwepo wa vyombo vya habari. Huu ni utashi wa Baba Mtakatifu Francisko mwenyewe kwani anataka kuzungumza na ndugu zake Maaskofu katika uhuru kamili, kwa kuuliza maswali na kujibu maswali kutoka kwa Maaskofu wenzake. Huu ni mkutano wa kidugu miongoni mwa Maaskofu wanapotekeleza dhamana yao ya kuongoza, kufundisha na kuwatakatifuza watu wa Mungu.

Padre Lombardi anakaza kusema, mara nyingi Baba Mtakatifu Francisko anapokuwa kwenye hija za kitume, anapenda kupata nafasi ya faragha na Maaskofu mahalia ili kuweza kufahamiana kwa karibu zaidi, kuzungumza na kushirikishana mang’amuzi na changamoto za maisha na utume wa Kanisa la kiulimwengu na Makanisa mahalia. Hivi ndivyo alivyofanya alipokuwa kwenye hija yake ya kitume Barani Afrika, Amerika ya Kusini, Cuba na Italia katika kipindi cha miaka miwili iliyopita.

Baba Mtakatifu Francisko ni kiongozi ambaye anapenda kushirikiana kwa dhati kabisa na tasnia ya habari. Yuko tayari kuhojiwa na wadau mbali mbali wa habari. Lakini yuko makini sana, anapotaka kuzungumza na ndugu zake katika Urika wa Uaskofu. Hapa mkazo ni uhuru kamili wa maaskofu wenyewe, umoja na udugu. Hivi ndivyo anavyofanya hata wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha kilichoko mjini Vatican. Pale ambapo Baba Mtakatifu anataka kuteta na ndugu zake, vyombo vya habari vinapisha na kukaa pembeni!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.