2016-07-23 17:55:00

Kusali ni sanaa inayohitaji muda na nafasi!


Kila nchi na watu wote kijumla wanapenda maendeleo. Wanapokosa njia ya kupata maendeleo, wanatafuta na kujifunza toka kwa wengine siri ya mafanikio. Watu wanafanya hivyo kwa vile wanajitambua kuwa ni taifa na wanataka kulijenga taifa lao. Namna hii ya kutafuta siri za mafanikio inatakiwa pia kuigwa na watu wa dini katika masuala ya kiroho na kimaadili. Katika maisha ya Yesu, hasa kipindi kile cha miaka mitatu ya kuhubiri hadharani alipata mafanikio makubwa sana. Luka katika Injili yake, anamwonesha Yesu ni mtu mwema  yuko kwenye harakati za za kuwaponya watu, za kuwasaidia maskini na fukara.

Kadhalika ni Rabi au mwalimu mwema mwenye kuhubiri habari njema kwa mafundisho mazuri yanayokonga mioyo hadi umati mkubwa wa watu ulivutika kumfuata. Lakini Yesu anaoneshwa pia karibu mara ishirini na saba kuwa anasali sana na mara nyingi anajitenga kwenda upwekeni kusali. Hadi wanafunzi wakagundua siri ya mafanikio ya Yesu yalitokana na kusali.

Aidha, katika kipindi hiki cha kuwa na Yesu, wanafunzi walijisikia wameunda kikundi kilichokamilika na mwalimu wao anazo sifa kama za marabi wengine maarufu kama akina Yohane Mbatizaji, Eliya na Wafarisayo. Walijua pia kwamba sifa ya kila kikundi cha rabi yeyote kilitakiwa kiwe na sala ya pekee inayowatambulisha na kuwatofautisha na wengine, kama ilivyo “Wimbo wa Taifa” (national anthem) unaotofautisha nchi moja na nyingine. Lakini tatizo likaja, kuwa wasali namna gani.

Kwa hiyo wanafunzi hawa walimwendea Yesu na kumwomba awafundishe sala ya kikundi. Hapo Yesu anachukua mwanya huo siyo kuwafundisha kusali, bali anawapendekezea namna gani ya kusali ili ijulikane kuwa ni sala mbele ya Mungu.  Tunaambiwa kwamba wanafunzi wakamsubirisha hadi alipomaliza kusali ndipo, “mmoja katika wanafunzi wake alimwambia,“Bwana tufundishe sisi kusali kama vile Yohane alivyowafundisha wanafunzi wake.”  

Pendekezo la kwanza Yesu anawaambia: “Msalipo semeni Baba [yetu uliye mbinguni]. Huu ndiyo mwelekeo anaotakiwa awe nao mtu katika sala, yaani kama mkao mkao wa maongezi ya mtoto na mzazi wake. Baba ni jina linalonipa picha gani ya mahusiano ninayo kati yangu na mzazi. Sala siyo tafakari ya sala ya moyo, au kutafakari biblia, bali ni kuongea au kuzungumza na Baba. Kusudi lake, mimi pamoja na Baba tuweze kuyaona kwa pamoja maisha na matatizo yangu. Neno la Baba linaweza kujibu maswali na matatizo ninayomtolea.

 

Katika Injili Yesu anazungumza karibu mara 182 juu ya Mungu kama Baba mwema. Kwa hiyo haitakiwi kumwogopa, bali kuonesha upendo na heshima, nidhamu na kuwa na mipaka ya Mwana na baba. Kwa hiyo sala inatufanya tumwone Mungu kama Baba ambaye daima anatanguzana na mwanae katika safari ya maisha yetu na anayetutakia tufurahi. Ama kweli hakuna mwingine kama Baba. Mapato ya furaha hiyo yananifanya nijisikie kuwa ni mwana wake, na hivi nitajitahidi nifanane naye katika maisha yangu na niwaone wengine wote kuwa ni waana wake pia, kwa kuwaheshimu na kuwapenda. Aidha kutokana na mtazamo huo yanafuata mambo mengine katika maisha yangu, hususani kutambua kuwa huyo Baba ni mtakatifu na anafanya mambo ya ajabu. Ndiyo maana utamsifu na kusema:

Jina lako litukuzwe (mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.] kutukuza maana yake, kumhusudu, kumshabikia, ni kuishi, ni kupokea sera zake na kuzitangaza kwa wengine. Kwa hiyo anayepokea na kuishi mapendekezo ya Baba, anakuwa mtu wa pekee kwani anafanana na huyo Baba akionesha kwamba ulimwengu unaumbwa naye. Mwana hulitukuzisha jina la Baba ulimwenguni na huu ndiyo uinjilishaji. Ulimwengu unajengwa na Mwana yule anayefanana na Baba yake yaani wewe. Unapoinjilisha jina lake, hapo unajenga na kueneza utawala wake ambao unataka uenee duniani kote unaposema:

Ufalme wako uje: Kwa hiyo, sala inatufanya tutambue tunafanya nini hapa ulimwenguni au tunaujenga utawala wa aina gani hapa duniani. Sala inatufanya tutambue waziwazi kama tunajenga ulimwengu tulioutunga sisi wenyewe kwa ujanja ujanja wetu, kwa ufisadi, kwa udhulumu, kwa uhujumu na unyanyasaji au tunajenga ulimwengu wa waana wa Mungu wanaopendana bila mipaka na masherti. Huu ndiyo ulimwengu tunaoalikwa kuunda wakati wa sala. Tukishamwona Mungu kama Baba yetu, yeye atatupa jicho la kuwaona waana wake wote kama anavyowaona yeye. Hiyo ndiyo maana ya ombi lifuatalo ambalo linatufanya tuwe na mahusiano yafaayo na mali yote ya Mungu yaliyo ulimwenguni yaani:

Utupe siku kwa siku riziki yetu:. Kila siku mtu anahitaji chakula au kupata riziki yake. Kwa hiyo kama mmoja anajimilikisha peke yake chakula cha mwaka mzima huyo hawezi kusali Baba yetu, kwani anajikusanyia hata chakula cha ndugu zake wanaohitaji. Kwa hiyo sisi tunaposali tunafahamu kwamba sisi sote pamoja na ndugu wengine ni watoto wa Baba mmoja, na tumealikwa kukaa hapa duniani na mali yote ni ya Baba. Kumbe tunapoacha kusali hapo tunausahau ukweli huo. Aidha, kwa sababu tunakosea katika hilo, sisi binadamu tunakoseshana sana raha hapa duniani na hiyo ndiyo inayoitwa dhambi. Kwa hiyo tumwombe Mungu atupe raha, tunaposali maneno haya:

Utusamehe dhambi zetu, kwa kuwa sisi nasi tunamsamehe kila tumwiaye.: Hapo haimaanishi kwamba tukitenda dhambi Baba anakasirika na atatuadhibu la hasha, bali msamaha maana yake ni kutufanyia kila kitu kitakachotupelekea kwenye raha, yaani atatutumia malaika atakayetuongoza katika njia ya furaha. Kwani dhambi ni kuchepuka toka kwenye njia inayotuongoza kwenye raha na kuelekea kwenye machungu. Kumbe hata sisi tunaweza kuwa malaika wa kuwasaidia wengine warudi kwenye njia sahihi itakayowaongoza wengine kwenye furaha ya kweli ya maisha. Huu ndiyo msamaha wa Mungu. Tunasali Baba yetu, kusudi tusilipizane kisasi, bali kusameheane, yaani kuwasaidia wengine kurudi tena barabara nzuri itakayowapatia tena furaha yao. Ninaposali namwomba Mungu anitumie malaika wa kuniongoza njia sahihi, nami nitajitahidi kuwa malaika kwa ndugu zangu na kwa wale walionitendea vibaya.

Usitutie majaribuni [lakini tuokoe na yule mwovu]. Tafsiri sahihi ya neno la kigiriki eiferein ni Usituingize ndani ya majaribu na siyo kishawishini kama tunavyosali. Kuna majaribu yanayotokana na hali yetu halisi ya kibinadamu yaani kuiweka imani yetu katika mazingira magumu, yanayoweza kututisha kiasi cha kutufanya tumdharau, au kumtukana Mungu  na kuona kama hayuko. Kumbe sala inatufanya tufahamu kuwa Mungu ni Baba. Katika sala tunaweza kumwonesha Mungu udhaifu wetu na kutufanya tusijikie tuko karibu naye zaidi. Sala inatufanya tujisikie tuko na Mungu katika majaribio kama alivyojisikia Yesu Getsemani alipoomba “Kikombe hiki nisikinywe,” ni sawa na kusali “Usiniingize katika majaribu.” Kwa hiyo ninapomwomba Mungu kutoniingiza majaribuni, naye ndiye anayenipa maana ya uwepo wangu.

Kisha Yesu anasema: “Nami nawaambia: Ombeni, nanyi mtapewa, tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa.” Huu ni msisitizo zaidi juu ya sala inayodai muda, siyo shauri la maneno tu yaliyopangwa, bali tunahitaji muda hadi pale unapoweza kupata zawadi anayotaka kutupatia Mungu pamoja na Roho wake. Kama anavyosema Yesu: “Baba atawazawadia Roho Mtakatifu hao wamwombao.” Zawadi hiyo ya Roho ya Mungu ni upendo. Ili kuipata au kwa na mazingira ya kuwa na roho hiyo inabidi kusali. Baba yetu ndiyo sala kuu ya kikundi cha wakristu. Tumwombe Baba ili tuwe na Roho ya upendo na huruma kama Yeye tunapomwita Baba yetu.

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.