2016-07-22 08:47:00

Uturuki hali ni tete!


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, Vatican inafuatilia kwa umakini na wasi wasi mkubwa machafuko ya kisiasa nchini Uturuki baada ya jaribio la kutaka kuipindua Serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan kushindikana hivi karibuni na watu zaidi mia mbili kupoteza maisha na wengine wengi kukamatwa na kutiwa kizuizini.

Kardinali Parolin anasema katika mazingira kama haya hekina na ubinadamu vinapaswa kutawala; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa: maisha, utu, heshima na mafao ya wengi. Mambo haya yasipozingatiwa kikamilifu, itakuwa ni vigumu kwa Uturuki kuweza kuondokana na mzunguko wa kulipizana kisasi. Jumuiya ya Kimataifa inaendelea kuonesha wasi wasi wake kutokana na machafuko ya kisiasa nchini Uturuki yanayotishia demokrasia, haki msingi za binadamu na utawala wa sheria.

Kwa upande wake, Rais Erdogan anasema, jaribo la kutaka kuipindua Serikali halali iliyoko madarakani ni kosa la jinai na uvunjaji wa sheria za nchi. Anasema, wanajeshi waliotaka kuipindua Serikali yake wanaongozwa na Imamu Fetullah aliyehamia uhamishoni nchini Marekani kunako mwaka 1999 na kwamba, anaitaka Serikali ya Marekani kumrejesha Imam Fetulla nchini Uturuki ili sheria iweze kushika mkondo wake. Serikali ya Uturuki imetangaza hali ya hatari kwa muda wa miezo mitatu kadiri ya Katiba ya Nchi. Serikali inaendelea kuwatia mbaroni wale wote waliojihusisha na jaribio la kutaka kuipindua Serikali pamoja na kuchukua hatua madhubuti katika marekebisho ya uchumi, ili kuwavutia wawekezaji kutoka ndani na nje ya Uturuki.

Takwimu zinaonesha kwamba, hadi sasa Viongozi wakuu wa Jeshi 113 kati ya 360 wamewekwa kizuizini; wanajeshi 262 pamoja na wanajeshi wa Polisi 900 wamefukuzwa kazi. Wakufunzi 95 kutoka Chuo Kikuu cha Istanbul wamesimamishwa kazi. Kuna watu wengi wanaokimbia kutoka Uturuki kwa kuhofia usalama wa maisha yao. Serikali ya Uturuki inazituhumu nchi za kigeni kwa kushiriki katika jaribio la kutaka kupindua Serikali yake ingawa hata Serikali hizi nazo zinaonya kuhusu umuhimu wa kulinda na kudumisha haki msingi za binadamu nchini Ururuki.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.