2016-07-22 09:34:00

Mt. Maria Magdalena shuhuda wa Huruma ya Mungu!


Mama Kanisa tarehe 22 Julai 2016 ameadhimisha kwa mara ya kwanza Siku kuu ya Mtakatifu Maria Magdalena shuhuda wa huruma ya Mungu kama alivyoagiza Baba Mtakatifu Francisko wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Lengo la Baba Mtakatifu katika maadhimisho haya ni kuwasukuma waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari kwa kina na mapana, ili hatimaye kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya wanawake katika mchakato mzima wa Uinjilishaji mpya, ili binadamu wengi waweze kuguswa na ukuu wa huruma ya Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anamwita Maria Magdalena kuwa ni mtume wa mitume “De apostolorum apostola” anayejipambanua kuwa ni shuhuda wa huruma ya Mungu “testis divinae misericordiae”. Kardinali Robert Sarah, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa anasema Mtakatifu Maria Magdalena alimpenda Kristo wakati wa uhai wake, akashuhudia akiteswa, kufa kuzikwa na kufufuka kwa wafu, alipokwenda asubuhi na mapema kule makaburini akakuta kaburi li wazi, Kristo Yesu amefufuka.

Mtakatifu Maria Magdalena anawahamasisha waamini kumtafuta Kristo katika maisha yao, ili waweze kumpenda kwa njia ya huduma kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii! Waweze kumsikiliza kwa makini kwa njia ya Neno la Mungu ili liweze kuwa ni taa inayoyaangazia mapito yao ya maisha! Waweze kumwabudu katika Sakramenti kuu ya Ekaristi Takatifu kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko.

Mtakatifu Maria Magdalena alikuwa ni mfuasi wa kwanza aliyemwabudu Kristo Mfufuka, dhamana inayoendelezwa na Mama Kanisa katika Liturujia ya Kanisa na Ibada mbali mbali zinazoadhimishwa na Mama Kanisa ili kumpatia Mwenyezi Mungu ukuu wake na mwanadamu kutakatifuzwa. Waamini wajenge utamaduni anasema Baba Mtakatifu Francisko wa kumsifu, kumtukuza, kumtumikia na kumwabudu Mwenyezi Mungu asili ya wema na utakatifu wa maisha.

Kumwabudu Mungu maana yake ni kumsikiliza kwa makini, kujadiliana naye kwa njia ya sala na hatimaye, kumwachia moyo wako ili aweze kuujaza kwa wema na baraka zake! Kwa njia hii, waamini wataweza kujifunza kupenda na kuhudumia kama alivyofanya Kristo Yesu katika maisha yake hapa duniani. Mtakatifu Maria Magdalena anawasaidia waamini kumwabudu, kumtangaza na kumshuhudia Kristo Mfufuka! Anaonesha ujasiri wa kutoka katika ubinafsi, ili kumtafuta Kristo Mfufuka, anayemkirimia mageuzi makubwa na utume katika maisha yaani kuwa ni Shuhuda wa Kristo Mfufuka! Hapa mkazo ni kuabudu na kuhudumia bila ya kujibakiza anasema Kardinali Robert Sarah kama tafakari yake kwa Siku kuu ya Mtakatifu Maria Madgalena mtume wa mitume!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.