2016-07-22 10:57:00

Mama Theresa wa Calcutta: Tuwapende wasiopendeka!


Mama Theresa wa Calcutta anatarajiwa kutangazwa kuwa Mtakatifu hapo tarehe 4 Septemba 2016, kielelezo na shuhuda wa huruma ya upendo wa Mungu unaomwilishwa kwa wagonjwa, maskini na wote wanaosukumwa pembezoni mwa jamii kwani upendo kwa jirani ndicho kipimo ambacho Yesu atakitumia siku ya mwisho kuwahukumu wazima na wafu! Maskini ni kundi lisilopendwa na wengi, kumbe hili ndilo kundi ambalo Mama Theresa wa Calcutta anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha upendo wao kwao.

Huu ni muhtasari wa kitabu ambacho kimeandikwa kwa heshima ya Mama Theresa wa Calcutta na Baba Mtakatifu Francisko kukiandikia dibaji yake! Baba Mtakatifu anawataka vijana wanaoshiriki maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kuwa ni vyombo na mashuhuda wa ujenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu kwa kufutilia mbali mantiki ya utengano na ubaguzi unaoendelea kupaliliwa na wengi duniani. Vijana wawe na ujasiri wa kuachana na tabia ya woga usiokuwa na mvuto wala mashiko na badala yake wawe ni mashuhuda na vyombo vya huruma na mapendo kwa maskini na wahitaji zaidi.

Mama Theresa wa Calcutta anakaza kusema, Ukoma na Kifua kikuu ni magonjwa ambayo hayawezi kufua dafu kwa upweke hasi unaoweza kumfanya mwanadamu kuchungulia na hata wakati mwingine kuonja kaburi! Upweke ni chanzo cha mipasuko ya kijamii, ukosefu wa amani, vita na majanga yanayomwandama mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu Francisko katika dibaji ya kitabu hiki anakazia mambo mafuatayo: Sala, upendo, huruma, familia na vijana. Anakumbusha kwamba, Kanisa katika maisha na utume wake linaendeleza kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Kristo Yesu na kwamba, kuna maskini wanaohitaji kuonjesha huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.

Mama Theresa wa Calcutta anawahamasisha waamini kujichotea nguvu ya huruma na upendo katika kisima cha: Sala, Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu na maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, ili kuweza kumwilisha sala katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Sala iwawezeshe waamini kukutana na kuzungumzana na Kristo Yesu; kuomba rehema na neema ili kuwa kweli ni watu wanaoweza kuthubutu kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani zao; kwa kuwaangalia wote kwa jicho la upendo linalopyaisha maisha ya watu!

Baba Mtakatifu anasema, upendo ni fadhila inayomwezesha mwamini kuwa kweli ni Msamaria mwema kwa jirani yake anayeogelea katika shida na magumu ya maisha: kiroho na kimwili. Upendo uwawezeshe waamini kuwa ni mashuhuda wa huruma inayoganga na kuponya madonda na majeraha ya maisha ya mwanadamu; ni ushuhuda wa faraja ya Mungu kwa madonda ya binadamu! Yote haya yanawezekana ikiwa kwama mwaminifu amefungamanisha maisha yake na Kristo Yesu, tayari kushuhudia uwepo na ukaribu wa Mungu mwingi wa huruma kwa waja wake!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kutafakari kwa makini huruma ya Mungu na kuimwilisha katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili tayari kupambana na umaskini, ujinga na maradhi mambo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu. Maskini ni kundi ambalo linaonjeshwa kwa namna ya pekee huruma ya Mungu, kumbe, waamini wawe kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Mama Theresa wa Calcutta aliyaandika matendo ya huruma: kiroho na kimwili katika maisha na utume wake, yakawa ni chachu ya utakatifu wa maisha, kumbe, ni jambo linalowezekana hata kwa waamini wengine kuiga mfano huu bora! Mama Theresa alionesha karama na utajiri wa kimama, akawapokea na kuwahudumia watu wote pasi na ubaguzi. Alikuwa na jicho la pekee hasa kwa vijana waliokuwa wanaishi katika mazingira magumu na hatarishi baada ya familia zao kusambaratika kutokana na sababu mbali mbali.

Bikira Maria ni mfano wa Umama unaoguswa na mahangaiko ya wengine, tayari kuyajibu kwa njia ya huduma makini! Waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wanahamasishwa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya faraja ya Mungu kwa familia zao kwa njia ya sala. Familia inahitaji kusimikwa katika upendo, umoja na kufanya kazi kwa juhudi, bidii na maarifa! Kwa kutekeleza yote haya, familia zinakuwa ni zawadi kubwa inayoweza kutolewa kwa Kanisa!

Mama Theresa wa Calcutta anawataka vijana kwa namna ya pekee kujenga maisha na uwepo wao kwa kumzunguka Kristo Yesu, ufunuo wa Huruma ya Mungu; mwamba thabiti na mwaminifu katika ahadi zake hata kama mwanadamu atakengeuka na kuasi. Baba Mtakatifu anawataka vijana wa kizazi kipya kukita maisha yao katika matumaini na kamwe wasithubutu kutoa nafasi kwa wajanja wachache kupoka matumaini yao, bali waendelee kushikamana na kumpenda Mungu; huku wakijenga madaraja yanayowaunganisha watu, kwa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini na wahitaji zaidi.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka Vijana wawe na ujasiri wa kupambana na changamoto za maisha, daima wakiwa na malengo ya juu pamoja na kuwashirikisha vijana wenzao fursa na mafanikio ya maisha. Vijana wa kizazi kipya warutubishe maisha yao kwa njia ya Neno la Mungu, Sakramenti na Sala ili kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu katika medani mbali mbali za maisha. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawatakia watu wote amani na furaha ya huruma ya Mungu iweze kutawala duniani kwa maombezi ya Mama Theresa wa Calcutta!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.