2016-07-21 15:00:00

Mawasiliano na athari zake katika maisha na utume wa familia Afrika!


Askofu Emmanuel Badejo, Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano ya Jamii Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, CEPACS akitoa mada kwenye mkutano wa 17 wa SECAM unaoendelea huko Luanda, Angola kwa kuongozwa na kauli mbiu “familia Barani Afrika: Jana, Leo na Kesho kadiri ya mwanga wa Injili” anasema familia ya Mungu Barani Afrika inakabiliwa na changamoto nyingi kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari; mambo ambayo yanahatarisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia Barani Afrika.

Familia ni kiini cha jamii, lakini ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia ya habari yamechangia kuvuruga muundo wa mawasiliano, dhamana na wajibu wa wazazi na walezi katika mawasiliano ya jamii. Kanisa linatambua na kuthamini familia kama kitalu cha maisha, mahali pa kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Mitandao ya kijamii anasema Askofu Badejo inaleta changamoto kubwa katika maisha ya kiroho, kimaadili na kiutu; kitamaduni, kidemokrasia, haki msingi za binadamu, usalama wa kitaifa na kimataifa sanjari na maahusiano ndani ya familia na jamii katika ujumla wake.

Kumbe, Kanisa haina budi kukazia umuhimu wa kudumisha ukweli, maadili na utu wema katika matumizi ya mitandao ya kijamii. Mitandao hii imekuwa ni nafasi yakuingiza siasa, tamaduni na mitazamo ambayo wakati mwingine inasigana na maadili, utu na heshima ya familia ya Mungu Barani Afrika! Anasema, mfano wa utamaduni wa kifo, ubinafsi na upweke, ulaji wa kupindukia ni mambo ambayo yamesambazwa kwa kasi kubwa Barani Afrika kwa njia ya mitandao ya kijamii na madhara yake yanajionesha kwenye maisha na utume wa familia.

Leo hii kuna watu wanadai kuwa ndoa za watu wa jinsia moja ni sehemu ya haki msingi za binadamu, lakini wanasahau mpango wa Mungu katika maisha ya binadamu! Uzazi kwa njia ya chupa na utoaji mimba ni mambo ambayo yanakuja kwa kasi ya ajabu hata katika familia za kiafrika kwa kisingizio cha haki msingi za binadamu na uzazi salama. Watu wanajengewa hoja ya kujiamini na uhuru usiokuwa na mipaka matokeo yake wanajikuta wapweke na wakavu katika maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni. Mambo yaliyokuwa yanakatazwa kama sehemu ya maadili na utu wema, leo hii ni ruksa kwa kila mtu, matokeo yake utii, uaminifu, udumifu, malezi na nidhamu vimepungua sana katika jamii.

Uhuru usiokuwa na mipaka ni matokeo pia ya Ukanimungu unaotaka kumweka Mwenyezi Mungu pembezoni mwa maisha na vipaumbele vya binadamu. Kimsingi watu wanataka kurahisisha maisha kwa kutafuta njia za mkato! Kumbe, kuna haja ya kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia Injili ya familia inayoambatwa katika Injili ya uhai na huruma ya Mungu! Wazazi na walezi watekeleze vyema dhamana na wajibu wao na Kanisa Barani Afrika liwe karibu zaidi na vijana wa kizazi kipya ili kuweza kuwafunda.

Tunu msingi za maisha ya ndoa na familia ziimarishwe na kudumishwa kwa katekesi makini na endelevu. Hapa kuna haja kwa familia ya Mungu Barani Afrika kuwa na Siku ya Familia Barani Afrika, ili kukazia tunu msingi za Injili ya familia kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wanaoendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Kanisa Barani Afrika linapaswa kutambua ajenda zinazofichika katika sera na misaada ya kiuchumi, ili kuifichua kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu Barani Afrika. Kanisa halina budi kuwekeza katika njia za mawasiliano ya kijamii Barani Afrika ili kusaidia kuwafunda watu wa Mungu katika imani, maadili na utu wema.

Kanisa Barani Afrika liwaandae wataalam watakaosaidia kufanya tafiti kuhusiana na masuala nyeti ya maisha na utume wa familia Barani Afrika, ili kusimama kidete: kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya familia. Kwa njia hii, Kanisa halina budi kuwa kweli ni sauti ya kinabii kwa kusimamia: utu, heshima, haki msingi za binadamu na mafao ya wengi.

Katekesi awali na endelevu kuhusu tunu msingi za maisha ya ndoa na familia haina budi kupewa kipaumbele cha pekee Barani Afrika. Wazazi na walezi wahusishwe kikamilifu katika malezi na makuzi ya watoto wao sanjari na kuhamasisha umoja na mshikamano kati ya familia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia. Viongozi wa familia wawe ni mfano bora wa maisha ili kukuza na kujenga tunu bora za maisha ya ndoa na familia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.