2016-07-21 15:18:00

Hayati Askofu mkuu Zymowski alikuwa ni mtu wa huduma!


Askofu mkuu Waclaw Depo wa Jimbo kuu la Czestochowa, katika mahubiri ya Ibada ya Misa ya mazishi ya Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya, Jumanne tarehe 19 Julai 2016 amesema, Marehemu Askofu mkuu Zimowski aliishi kwa ajili ya huduma. Na wala si kuwa ajili ya kuhudumiwa. “Non mistirari sed mistirare”. Huu ni muhtasari wa maisha yake hapa duniani. Ibada ya Misa imeongozwa na Kardinali Stanislaw Dziwisz, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Cracovia na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Jimbo Katoliki la Radom nchini Poland. Monsinyo Jean-Marie Mupendawatu aliwakilisha Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa ajili ya wafanyakazi katika sekta ya afya.

Dr. Franco Balzaretti, Makamu wa Rais Chama cha Madaktari Wakatoliki Italia anasema Marehemu Askofu mkuu Zimowski ni kiongozi aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma makini kwa wagonjwa kama njia ya kutangaza na kushuhudia Injili ya huruma ya Mungu kwa waja wake; akawa ni mfano bora wa kuigwa katika huduma kwa wagonjwa sehemu mbali mbali za dunia. Alikuwa ni shuhuda na mwalimu aliyemwilisha mafundisho yake kuhusu Injili ya maisha katika uhalisia wa maisha ya watu.

Askofu mkuu Zimowski daima aliwaasa wafanyakazi katika sekta ya afya kutekeleza wajibu wao barabara kwa kutambua kwamba, Mungu ni upendo. Dhamana hii pia ilipaswa kushuhudiwa kama kielelezo cha imani tendaji, ili kuwapatia wagonjwa na watu waliokuwa wanateseka matumaini katika hija ya maisha yao ya kila siku. Walipaswa kutangaza na kushuhudia ukweli, amani na upendo kwa watu wenye kiu ya huruma na upendo wa Mungu unaopokelewa kwa njia ya imani. Ikumbukwe kwamba, imani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wajibu wa kumwona Mwenyezi Mungu kwa njia ya shida na mahangaiko ya jirani.

Mateso na mahangaiko ya mwanadamu katika ugonjwa ni tema ambayo mara kwa mara Hayati Askofu mkuu Zimowiski aliifanyia tafakari katika maisha yake na kuwataka waamini kukabiliana na changamoto hii katika mwanga wa imani, matumaini na mapendo. Katika mazingira kama haya imani ni muhimu sana na wala haina mbadala. Kwa njia hii, waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema wanaweza kusimama kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai; utu na heshima ya binadamu.

Katika ulimwengu mamboleo changamoto dhidi ya Injili ya uhai zimeongezeka maradufu, kiasi cha maisha ya mwanadamu kuwekwa rehani kwa kisingizio cha haki msingi za binadamu, uhuru  na uzazi salama; mambo ambayo kimsingi yanakumbatia utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba na kifo laini. Watu wanasahau kwamba, mtoto ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, lakini kuna watu wanadhani kwamba,  mtoto ni kama bidhaa inayoweza kununuliwa dukani, ndiyo maana kuna watu wanaotafuta watoto kwa udi na uvumba, kiasi hata cha kuanza kuzalisha watoto kwenye chupa! Wafanyakazi wa sekta ya afya, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Mapambano haya yanaweza kufanikiwa ikiwa tu watu wataungana katika umoja, upendo na mshikamano.

Chama cha Madaktari Wakatoliki Italia wanasema, kifo cha Askofu mkuu Zimowski kimeacha pengo kubwa ambalo halitakuwa ni rahisi kuweza kuzibika kwa urahisi. Daima alipenda kukazia kwamba, Mwenyezi Mungu anawapenda watu wake na kamwe hawezi kuwatelekeza. Ni matumaini yao kwamba, hata Marehemu Askofu mkuu Zimowski ataendelea kuwa mwombezi wao huko mbinguni kama alivyokuwa hapa duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.