2016-07-20 08:59:00

Wakleri ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu!


Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri, katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anapenda kuwakumbusha Wakleri wenzake kwamba, kabla hata ya kuwekewa mikono na kuwa ni: Mashemasi, Mapadre na Maaskofu wao ni waamini waliobatizwa kwa maji na Roho Mtakatifu na kwamba, utambaulisho wao wa kwanza ni waamini na wafuasi wa Kristo Yesu. Kwa kuwekwa wakfu katika Sakramenti ya Daraja takatifu wanakuwa ni mashuhuda, vyombo na wahudumu wa Mafumbo ya Kanisa.

Kwa namna ya pekee ni wahudumu wa Sakramenti za huruma ya Mungu, yaani Ekaristi Takatifu inayowajalia waamini chakula cha njiani katika hija ya maisha yao hapa bondeni kwenye machozi pamoja na Sakramenti ya Upatanisho inayowaonjesha waamini, huruma, upendo na msamaha wa Mungu katika maisha yao, tayari hata wao kuwa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu inayomwilishwa katika vipaumbele vya maisha yao!

Kutokana na uzoefu na mang’amuzi ya maisha, Wakleri kwa namna ya pekee ni viongozi wa Jumuiya ya waamini katika safari ya maisha yao ya kiroho; dhamana wanayoitekeleza kwa kutambua kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma ya mapendo kwa ajili ya kuwasindikiza waamini katika maisha yao kwa njia ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa katika ujumla wake. Kwa njia hizi, waamini wote wanaweza kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao anasema Kardinali Beniamino Stella.

Wakleri wajitahidi wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu kwa watu wao na kamwe wasimezwe na malimwengu yanayoweza kuweka mchanga huduma wanayoitoa kwa ajili ya familia ya Mungu. Maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa yawasaidie kwanza kabisa Wakleri wenyewe kuchuchumilia na kukita maisha yao katika safari ya utakatifu wa maisha. Watambue kwamba, njia ya kwenda mbinguni wataweza kuifikia kwa kutumia ngazi ya utakatifu na upendo katika shughuli za kichungaji.

Wakleri wawe mstari wa mbele kupiga magoti kwenye Kiti cha huruma ya Mungu ili kufanya toba na kuomba msamaha wa dhambi zao, changamoto makini inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko ambaye yuko tayari daima kupiga magoti ili kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Baba Mtakatifu anatambua nguvu na karama alizojaliwa na Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu lakini pia anafahamu fika udhaifu na mapungufu yake ya kibinadamu, ndiyo anakimbilia mara kwa mara Uso wa huruma ya Mungu ili aweze kupata msamaha, faraja na maondoleo ya dhambi.

Kardinali Stella anakaza kusema, kwa njia ya Kanisa, Wakleri wanapata fursa ya kuonja huruma na msamaha wa dhambi zao kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kwa njia hii, wanaweza kuwa na moyo mnyofu, tayari kuwapokea na kuwasaidia wale wote wanaokimbilia huruma ya Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani, ili kugangwa na kuponywa na huruma ya Mungu. Lengo ni kuwawezesha waamini kupata furaha ya ndani kwa kuondolewa dhambi zao, na hatimaye, kukumbatiwa na Mwenyezi Mungu. Wakleri wanebarikiwa kwa njia ya huruma ya Mungu, ili nao waweze kuwabariki ndugu zao katika Kristo.

Wakleri wakumbuke kwamba wanapendwa na Mungu, ili nao waweze kuwagawia wengine upendo huu, ili kweli maisha yao yaweze kuakisi huruma ya Mungu inayowaambata daima wanapokuwa katika shughuli za kitume, wanapoadhimisha Mafumbo ya Kanisa, wanapokuwa likizoni au wanapotoa katekesi au kuwahudumia waamini walei katika maisha na utume wao. Utenzi wa huruma ya Mungu unapaswa kuwa ni sehemu ya vinasaba na maisha ya Wakleri katika huduma kwa familia ya Mungu, lakini jambo la msingi ni kukita maisha katika toba na wongofu wa ndani!

Wakleri wanahamasishwa kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu katika huduma za kichungaji; kwa kuhamasisha pia majadiliano ya kiekumene na kidini, kwani huruma ya Mungu inawaambata wote pasi na ubaguzi kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Huruma ya Mungu iwaambate vijana na watoto pamoja na familia, lakini zaidi kwa zile familia ambazo zimekumbwa na misiba na magonjwa. Hawa ni watu wanaoguswa kwa namna ya pekee na uwepo wa Wakleri katika nyakati kama hizi.

Wakleri waoneshe pia ari na moyo wa ukarimu kwa wageni pamoja na kushiriki kikamilifu katika maisha ya watu mahalia! Padre ameteuliwa kutoka kwa watu kwa ajili ya watu kuhusiana na mambo matakatifu! Wakleri wema na watakatifu ni mashuhuda wa neema na huruma ya Mungu inayoendelea kufanya miujiza katika maisha ya watu, lakini Wakleri wakatili ni hatari sana katika maisha na utume wa Kanisa. Wakleri wawe kweli ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani, upendo na msamaha katika jamii ambamo kuna vita, kinzani, utengano na mipasuko mikubwa ya kidini, kikabila, kisiasa na kijamii. Huruma, msamaha na upatanisho, vimwilishwe kwanza kabisa katika maisha ya Wakleri wenyewe pale walipo kwa kujenga mahusiano mema na matakatifu na Wakleri wenzao pamoja na waamini walei.

Kardinali Stella anasema, huruma ya Mungu inapaswa kumwilishwa katika maisha na utume wa familia, kwa kujikita katika wosia wa kitume wa Baba Mtakatifu Francisko, “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Waamini wahamasishwe kuusoma, kuutafakari na kuumwilisha katika uhalisia wa maisha yao, ili kusimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya familia. Huruma ya Mungu ndiyo mantiki ya Wosia huu wa Baba Mtakatifu.

Katika shida na magumu ya maisha, huduma ya upendo unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu ni muhimu sana na kwamba, hapa Wakleri wanapaswa kuonesha kweli kwamba, wao ni majembe makini ya huruma ya Mungu kwa watu wake. Maisha yao, yawe ni kielelezo makini cha huruma ya Mungu na faraja kwa watu wake. Huruma ya Mungu imwilishwe katika maisha ya maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii anasema, Kardinali Beniamino Stella anapohitimisha wosia wake kwa Wakleri wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.