2016-07-19 12:08:00

Teteeni ukweli na iweni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu!


Shirika la Wadominikani kuanzia tarehe 16 Julai hadi 5 Agosti 2016 huko Bologna, Kaskazini mwa Italia, linaadhimisha mkutano mkuu wa Shirika, sanjari na maadhimisho ya Jubilei ya miaka 800 tangu kuanzishwa kwa Shirika hili ambalo limekuwa na mchango mkuu katika maisha na utume wa Kanisa. Shirika hili linaadhimisha mkutano huu sanjari na maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Wajumbe hawa baadaye watapata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Papa Francisko.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, anapenda kuchukua fursa hii kuwapongeza na kuwaombea karama na mapaji ya Roho Mtakatifu, daima wakikumbuka kwamba, huruma ya Mungu ndiyo nguzo kuu ya Kanisa. Maisha na utume wa Kanisa hauna budi kutekelezwa kwa kuzunguka nguzo hii msingi inayofumbata utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu na ushuhuda makini wenye mvuto na mashiko.

Thamani ya maisha na utume wa Kanisa unajidhihirisha kwa njia upendo na huruma inayowakirimia watu maisha mapya pamoja na ujasiri ili kuyaangalia ya mbeleni kwa matumaini. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, wafuasi wa Mtakatifu Domenico wanaofuata karama yake wataendelea kuwa mashahidi na vyombo vya msamaha na huruma ya Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; tayari kusimama kidete kulinda na kutetea ukweli; kushuhudia, kukiri na kumwilisha huruma ya Mungu katika maisha kama alama ya upole wa Mungu kwa waja wake, ili Jamii mamboleo iweze kugundua umuhimu wa mshikamano, upendo na msamaha.

Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wa matashi mema kwa Wadominikani wanaoadhimisha mkutano mkuu wa Shirika , Jubilei ya miaka 800 tangu kuanzishwa kwa Shirika sanjari na Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, kwa kuwaomba kumsindikiza katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa njia ya sala na sadaka zao. Kwa upande wake, Baba Mtakatifu anawakabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Rozari Takatifu na ya watakatifu wote kutoka katika familia ya Wadominikani. Anawapatia wajumbe wote wa mkutano mkuu baraka zake za kitume.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.