2016-07-19 14:39:00

Injili ya familia Barani Africa!


Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI katika Waraka wake wa Kitume, “Dhamana ya Afrika” “Africae Munus” anasema, familia ni Hekalu la uhai na chembe hai ya jamii na ya Kanisa. Hapa ni mahali ambapo watu hupata mafundisho ya msingi: kiroho, kimwili, kiutu na kijamii. Ni mahali pa kujifunza kupenda na kupendwa; kuheshimu na kuheshimiwa. Ni mahali pa ujenzi wa utamaduni wa msamaha, amani na upatanisho; mahali pa kujengana na kusaidiana katika kukabiliana na changamoto za maisha.

Kutokana na changamoto, matatizo na fursa mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo, Injili ya familia haina budi kulindwa, kukuzwa, kudumishwa na kushuhudiwa kama kielelezo cha imani tendaji. Ili kujenga na kudumisha umoja, upendo na mshikamano wa dhati, familia zinapaswa kujikita katika maisha ya Sala, tafakari ya Neno la Mungu na kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa; mambo yanayomwilishwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Familia za Kikristo ziwe ni tabernakulo ya Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Kanisa Barani Afrika linalo jukumu na kukuza na kudumisha utume wa familia kama sehemu ya mchakato wa kumwilisha Injili ya familia katika maisha ya waamini, ili waweze kuitangaza na kuishuhudia kwa njia ya maisha yenye mvuto na mashiko. Familia ya Kikristo inapaswa kuwa ni shule ya utakatifu, haki na amani; mahali pa kujifunzia tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu, kimaadili na kitamaduni. Hapa wanafamilia hawana budi kuinjilishwa, ili waweze kuinjilisha, kwa kuhakikisha kwamba, wazazi na walezi wanatekeleza vyema dhamana na majukumu yao katika maisha ya ndoa na familia.

Familia Barani Afrika inakabiliwa na changamoto kubwa zinazoendelea kuibuliwa na ulimwengu wa utandawazi pamoja na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kumbe, hapa Kanisa Barani Afrika halina budi kuibua mbinu mkakati wa utume wa familia Barani Afrika. Kardinali Arlindo Gomes Furtado, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Santiago de Cape Verde atazungumzia kwa kina na mapana changamoto hizi. Mwelekeo wa familia kutoka Barani Afrika ni mada inayochambuliwa na Askofu Emilio Sumbulelo wa Jimbo Katoliki Uije, Angola. Maendeleo ya sayansi na teknolojia ni changamoto kubwa katika maisha na utume wa ndoa na familia. Hii ni mada inayochambuliwa na Askofu Emmanuel A. Badejo, Mwenyekiti wa Tume ya Mawasiliano Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM.

SECAM inapojiandaa kuadhimisha Jubilei ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, inapaswa kusimama kidete katika kutekeleza dhamana na majukumu yake kwa familia ya Mungu Barani Afrika. Kardinali Philippe Ouedraogo kutoka Burkina Faso anawashirikisha wajumbe mbinu za kutaka kuimarisha SECAM ili kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu Barani Afrika. Baada ya sala, tafakari na mang’amuzi kuhusu maisha na utume wa familia Barani Afrika kadiri ya mwanga wa Injili, Mababa wa SECAM wataibuka na Ujumbe kwa ajili ya familia ya Mungu Barani Afrika.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican kwa msaada wa CANAA.








All the contents on this site are copyrighted ©.