2016-07-18 11:58:00

Vijana jibidisheni kumtafuta Mungu katika maisha yenu!


Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua umuhimu wa ujenzi wa umoja na mshikamano miongoni mwa vijana huko Marekani, Jumamosi, tarehe 16 Julai 2016 ametuma ujumbe kwa njia ya video kwa vijana waliokuwa wamekusanyika huko Washington DC., Marekani kwa ajili ya sala ya kiekumene. Tamasha hili lilikuwa limeandaliwa na kikundi cha sala na Uinjilishaji kijulikanacho kama “Nick Hall”.

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake anawaambia vijana kwamba, anatambua kile ambacho kiko mioyoni mwao; yale mambo yanayowasumbua na kuwasababishia kukosa amani na utulivu wa ndani. Kijana ambaye ametulia kama maji mtungini, huyu atazeeka angali kijana mbichi. Baba Mtakatifu anawauliza vijana swali la msingi, Je, ni mambo yepi yanayomsumbua kijana moyoni mwake? Baba Mtakatifu anawaalika vijana kuchangamkia nafasi za kukutana na vijana wenzao katika sala na tafakari ili waweze kupata majibu muafaka yatakayozima kiu ya matamanio katika maisha yao.

Baba Mtakatifu anasema, vijana katika hija ya maisha yao wajitahidi kukutana na Kristo Yesu, hapo watapata amani na utulivu wa ndani na kamwe hawatachanganyikiwa kwani Mwenyezi Mungu hawezi kumhadaa mwamini anayemtegemea na kukimbilia huruma na tunza yake. Baba Mtakatifu anawahakikishia vijana kwamba, Yesu anawasubiri kwani ndiye aliyepanda mbegu ya kumhangaikia katika maisha. Baba Mtakatifu anawatia shime kwa kusema kwamba, hawana kitu cha kupoteza! Anawataka kujaribu na baadaye, wamtwangie simu kumshirikisha siri ya urembo wa maisha yao ya kiroho!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.