2016-07-18 07:24:00

Mwenyeheri Kardinali Alojzije Stepinac


Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni aliunda Tume maalum inayowaunganisha wajumbe kutoka Vatican, Kanisa Katoliki la Serbia na Kanisa la Kiorthodox la Serbia ili kupembua kwa kina na mapana masuala ya kihistoria juu ya maisha na utume wa Mwenyeheri Kardinali Alojzije Stepinac, kabla, wakati na baada ya Vita kuu ya Pili ya Dunia. Tume hii imeundwa baada ya mikutano ya ushauri kutoka Vatican, Kanisa la Kiorthodox la Serbia pamoja na Baraza la Maaskofu Katoliki Serbia, ili kupata ufafanusi wa masuala mbali mbali ya kihistoria kabla ya kuendelea na mchakato wa kumtangaza Kardinali Stepinac kuwa Mtakatifu.

Tume hii imepewa dhamana ya kufanya kazi ya kisayansi huku ikizingatia mbinu za kisayansi katika masuala ya kihistoria kwa kuchunguza na kupembua nyaraka mbali mbali zinazopatikana kwa wakati huu kwa kuzingatia mazingira ya wakati ule. Taarifa inakazakusema, uchunguzi huu wa kisayansi hautaweza kuingilia mchakato wa kumtangaza kardinali Alojzije Stepinac kuwa Mtakatifu, kwani hii ni dhamana maalum ya Vatican na wala haina uhusiano na masuala ya kihistoria. Kutakuwepo na mikutano kadhaa inayotarajiwa kuhitimishwa katika kipindi cha mwaka mmoja kuanzia sasa. Wajumbe hawa wanatarajiwa kukutana tena huko Zagabria kuanzia tarehe 17 – 18 Oktoba 2016.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.