2016-07-18 07:10:00

Jengeni zaidi mshikamano wa kitaifa dhidi ya chuki na uhasama!


Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa katika tamko lake kuhusiana na shambulizi la kigaidi lililotokea hivi karibuni huko Nice, Ufaransa linasema ni matukio yanayoendelea kupandikiza simanzi na majonzi nchini Ufaransa na sehemu mbali mbali za dunia kwa muda mrefu sasa. Mauaji ya kigaidi ni vitendo ambavyo kamwe haviwezi kukubalika wala kuvumiliwa na wapenda amani duniani. Ufaransa imeshambuliwa wakati inasherehekea siku kuu ya umoja wa kitaifa. Maaskofu wanakumbusha kwamba, umoja na mshikamano wa kitaifa vitadumishwa kuliko hata wasi wasi wa mashambulizi ya kigaidi yanayoendelea kupandikiza utamaduni wa kifo kati ya watu.

Hivi ndivyo anavyosema Askofu mkuu Georges Pontier, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ufaransa. Katika Ibada ya Jumapili, tarehe 17 Julai 2016, Kanisa Katoliki limewakumbuka na kuwaombea Marehemu wote waliofariki dunia katika shambulizi la kigaidi lilofanyika huko mjini Nice. Jimboni Nice, kumefanyika maadhimisho ya kiekumene kwa ajili ya kuwakumbuka na kuaombea marehemu wa vitendo vya kigaidi.

Askofu Andrè Marceau wa Jimbo Katoliki la Nice amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa makini na kamwe wasikubali kuzamishwa katika kishawishi cha kutaka kulipiza kisasi, chuki, uhasama na ubaguzi au kujifungia katika undani wao. Haya ni mambo ambayo yanapaswa kuepukwa kwa gharama zote, ili kujenga amani na utulivu wa ndani!

Kwa upande wake, Patriaki Kirill wa Kanisa la Kiorthodox kwa Moscow na Russia nzima anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kufanya tafakari ya kina na mapana ili kuangalia kile kinachoendelea kutendeka katika ustaarabu wa mwanadamu. Kumekuwepo na vitendo pamoja na mashambulizi ya kigaidi dhidi ya watu wasiokuwa na hatia. Majibu ya maswali mengi yanayoulizwa kwa wakati huu yanaweza kupata jibu lake kutokana na maisha ya kiroho ambayo mwanadamu wa leo anataka kuyaendekeza.

Viongozi wa Shirikisho la Makanisa ya Kiinjili ya Kiluteri Duniani, wameitaka Jumuiya ya Kimataifa kujibu mashambulizi haya kwa kuwa na mwelekeo chanya zaidi, unaopania kujenga na kuimarisha umoja wa familia ya binadamu na kamwe isiwepo Jumuiaya inayotaka kupandikiza mbegu ya utamaduni wa kifo kwa njia ya vitendo vya kigaidi. Wakati huo huo, Baraza la Makanisa Barani Ulaya linawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujenga na kudumisha mazingira ya kuaminiana kwa kuoneshana ukarimu na mapendo na watu wote wenye mapenzi mema na imani tofauti bila ubaguzi.

Taarifa za vyombo vya ulinzi na usalama nchini Ufaransa zinasema kwamba, dereva wa lori la kifo ametambuliwa kuwa ni Bwana Mohamed Lahouaeij Bouhlel mwenye umri wa miaka 31 kutoka Tunisia aliyekuwa na kibali cha kuishi nchini Ufaransa. Alikuwa ni ameoa na watoto watatu na kwamba, taarifa zinaonesha kuwa hivi karibuni alikuwa na matatizo ya kifamilia baada ya kuachana na mke wake na wala hakuwa ni mchamungu sana kwa dini yake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.