2016-07-16 15:57:00

Monsinyo Gàbor Pintèr awekwa wakfu kuwa Askofu mkuu


Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, tarehe 15 Julai 2016 amemweka wakfu Monsinyo Gàbor Pintèr kuwa Askofu mkuu na Balozi wa Vatican nchini Bielorussia. Ibada hii imeadhimishwa kwenye Kanisa kuu la Vac nchini Hungaria na kuhudhuriwa na umati mkubwa wa familia ya Mungu kutoka Hungaria uliokuwa unaongozwa na Kardinali Peter Erdo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Budapest, Hungaria. Kumekuwepo na ujumbe wa kiekumene katika maadhimisho haya, kielelezo makini cha mchakato wa ujenzi wa umoja wa Kanisa la Kristo.

Katika mahubiri yake, Kardinali Parolin amesema, Mhusika mkuu katika Ibada hii ya Misa Takatifu ni Roho Mtakatifu anayemtia wakfu na kumtuma Askofu mkuu Pintèr kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kati ya watu wa Mataifa. Hii ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa na wala haipaswi kufungiwa kibindoni kana kwamba, ni mali ya mtu binafsi. Habari Njema ya Wokovu ni ujumbe wa furaha na faraja; upendo, msamaha na huruma ya Mungu inayogeuza chuki na uhasama kuwa ni chemchemi ya upendo; kifo kuwa ni mwanzo wa maisha mapya.

Askofu mkuu Pintèr anatumwa kutangaza na kushuhudia Mwaka wa Bwana uliokubalika kwa kuendelea kumuiga na kumfuasa Kristo mchungaji mwema na kiongozi mkuu wa Kondoo wake, anayepaswa kukita maisha yake katika amani, ukweli na maisha, ili kuweza kuwafikia watu wengi zaidi na kuwapatia faraja na huruma inayobubujika kutoka kwa Kristo mchungaji mwema.

Askofu anawekwa wakfu, kielelezo cha ukamilifu wa Daraja takatifu la Upadre na hivyo anakuwa ni kiungo kati ya Mungu na wanadamu. Kwa njia ya maisha yanayozamishwa katika sala, ataweza kuwasaidia watu wengi zaidi kukuza hamu na kiu ya kumfahamu, kumpenda na kumtumikia Mungu sanjari na kuendeleza ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani. Mamlaka ya Askofu yanajikita katika huduma inayopania pamoja na mambo mengine kujenga na kudumisha umoja wa Kanisa; kuratibu na kuongoza karama mbali mbali za familia ya Mungu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo, tayari kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini kwa kuanzia na Mapadre wake.

Askofu anapaswa kuonesha dira na njia yakufuata; kuwa ni kiungo cha umoja, upendo na mshikamano kati ya familia ya Mungu pamoja na kuendelea kuwaongoza hata wale wadhaifu; kwa kusikiliza kwa makini mateso na mahangaiko yao ya ndani, ili kuwainua tena na kuwapatia matumaini katika maisha na wito wao wa Kikasisi. Askofu awe na hekima na busara ili kuwakusanya wote chini ya mchungaji mmoja bila ya kuwaacha wala kuwatenga watu wake. Askofu aoneshe upendo wa dhati kwa Kristo na Kanisa lake, ili kuweza kuwa tayari kuwaimarisha ndugu zake katika imani, mapendo na matumaini.

Mshikamano wa upendo kati ya Askofu, Kristo Yesu na Kanisa lake unajionesha kwa namna ya pekee katika maisha ya sala, upendo wa kichungaji pamoja na kutumia madaraka yake kwa kuwajibika, haki, wema na upole. Askofu mkuu Gàbor Pintèr anaweka wakfu ili kuwa ni kiungo muhimu sana kati ya Kanisa mahalia na Kanisa la Kiulimwengu kwa kumwakilisha Khalifa wa Mtakatifu Petro katika nchi husika, ili kujenga na kuimarisha Kanisa mahalia kwa kudumisha umoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Askofu mkuu Pintèr anakuwa ni daraja kwa wale wanaotamani kuungana na Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake, huku wakiwa na kiu na hamu ya amani na wema. Anakuwa ni alama ya umoja na ushirikiano na watu wote wenye mapenzi mema kwa kujikita katika kulinda, kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu, hususan haki ya uhuru wa kuabudu. Askofu anakuwa ni chombo cha haki na huruma ya Mungu; msamaha na matumaini, daima akijitahidi kudumisha mafao ya wengi, haki, amani na maridhiano.

Kardinali Parolin amemhakikishia Askofu mkuu Gàbor Pintèr kwamba nchini Bielorussia atakutana na Jumuiya ya Mungu iliyo hai yenye furaha na shuhuda wa imani yake. Atakuwa na dhamana ya kujenga na kuimarisha umoja wa Wakristo kwa njia ya majadiliano ya kiekumene pamoja na kuisaidia kuendelea kuwazi kwa Jumuiya ya Kimataifa. Kama Askofu kwa njia ya maisha na matendo yake anapaswa kumtangaza Kristo kwa kuwa ni amana ya huruma ya Mungu inayobubujika kutoka katika Moyo Mtakatifu wa Yeu na chemchemi ya nguvu ya Roho Mtakatifu anayeunganisha Kanisa mahalia na Kanisa la Kiulimwengu katika mchakato wa kusaidiana na kuimarishana kama ndugu.

Askofu mkuu Pinter anatumwa kuwa ni mjumbe na chombo cha haki na amani kwa kujikita katika utawala wa sheria, ustawi na mafao ya wengi. Anapaswa kuwa ni chemchemi ya furaha na matumaini kwa ajili ya familia ya Mungu baada ya kukutana na Kristo Mfufuka. Anapaswa kujitahidi kuhakikisha kwamba, anapata mafanikio makubwa kadiri ya mapenzi ya Mungu, kwa kujiaminisha kwake na katika mpango wake wa upendo.

Kwa upande wake, Kardinali Peter Erdo akitoa salam na shukrani zake kwa Kardinali Pietro Parolin aliyeongoza Ibada ya kumweka wakfu Askofu mkuu Gàbor Pintèr anasema, imani ya Kikristo iko karibu na watu wote. Amri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu ni dhamana na wajibu wa kila Mkristo. Kwa njia ya Balozi wa Vatican kwenye Kanisa mahalia, familia ya Mungu katika nchi hiyo inashiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu kwa kushirikisha shuhuda za imani na tamaduni zao. Amemtakia heri na baraka Askofu mkuu Pintèr katika maisha na utume wake kama Balozi wa Vatican huko Bielorussia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.