2016-07-15 09:14:00

Mwaka mmoja tangu Papa Francisko alipotembelea Paraguay!


Kardinali Beniamino Stella, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri wakati wa ziara yake ya kikazi nchini Paraguay hivi karibuni, amepata nafasi ya kuzindua Jumba la Makumbusho lililopewa jina la Papa Francisko, kwenye Kanisa la Bikira Maria kupalizwa mbinguni. Amepata nafasi pia ya kuweza kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Paraguay kwa kuwataka kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa sanjari na kujikita katika mchakato wa majiundo awali na endelevu kwa Wakleri nchini Paraguay, ili kuwaimarisha katika utume wao, huku wakiendelea kuiga mfano wa Kristo Yesu, mchungaji mwema.

Kardinali Stella amekazia pia umuhimu wa Kanisa kuwa na mikakati ya majiundo endelevu kwa ajili ya Wakleri, vinginevyo, Wakleri wao watanyauka na kukata tamaa kwani maisha ya Kipadre yanapaswa kupaliliwa na kuwekewa mbolea ya maisha ya kiroho kwa njia ya majiundo awali na endelevu.

Baadaye Kardinali aliadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Wakleri, Watawa na vijana ambao wako njiani kutafuta wito wa maisha yao ndani ya Kanisa. Wote hawa wamekumbushwa kwa mara nyingine tena, wito uliotolewa na Baba Mtakatifu Francisko alipokutana na kundi hili la familia ya Mungu kutoka Paraguay. Amewataka kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa.

Akiwa nchini Paraguay, Kardinali Stella alitembelea Seminari kuu ya Kitaifa na baadaye alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Rais Horacio Cartes wa Paraguay, aliyempatia salama na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko anayeendelea kukumbuka kwa heshima kubwa hija yake ya kitume nchini Paraguay, mwaka mmoja uliopita.

Kardinali Stella akiwa ameambatana na Askofu mkuu Eliseo Antonio Arioti pamoja na baadhi ya Maaskofu mahalia, waliweza kutembelea Mashariki mwa Ciudad na huko wakapata nafasi ya kukutana na kuzungumza na  Wakleri pamoja na watawa wa Jimbo hili. Wakleri na Watawa wanaendelea kuhimizwa kwa namna ya pekee katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu kuwa kweli ni mashuhuda na wahudumu wa huruma ya Mungu. Hata Wakleri katika maisha yao, wanapaswa kuwa na viongozi wao wa maisha ya kiroho, dhamana wanayopaswa kuitekeleza hadi pale wanapoingia kaburini.

Kardinali Beniamino Stella akiwa nchini Paraguay alipata nafasi pia ya kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika Kanisa kuu la Caacupè. Katika mahubiri yake alijikita zaidi kwenye mfano wa Msamaria mwema, kwa kuonesha kwamba, upendo kwa jirani si dhana ya kufikirika inayoelea angani, bali ushuhuda wa maisha unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu: kiroho na kimwili. Hivi ndivyo Yesu alivyopenda na kufanya katika maisha na utume wake. Yesu alionesha ukarimu, akasamehe dhambi za watu; akaganga na kuponya magonjwa. Hata leo hii, familia ya Mungu inahamasishwa kuwa kweli ni shuhuda na chombo cha huruma ya Mungu katika ulimwengu mamboleo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.