2016-07-15 15:49:00

Madongo na majungu si mtaji, vinginevyo wengi wangeulamba!


Katika kijiji kimoja cha Betania kilichoko umbali wa km tatu hivi kutoka Yerusalemu kulikuwa na familia moja ya watu watatu tu, kaka mmoja aitwaye Lazaro na dada wawili Martha na Maria. Familia hii siyo ya kijijini kama ilivyokuwa Kafarnaumu au Nazareti, bali ni ya mjini Yerusalemu makao makuu ya dini na serikali Kwa maneno mengine hawa walikuwa ni watu wa mjini kwani mjini kisomo, shamba kilimo. Hapo walikaa wanasheria, wafarisayo, makuhani waliojaa ukiritimba na wanyanyasaji wa maskini na wenye kuwabagua wanawake nk.

Yesu alikuwa huko huko akipambana nao, akiwatetea wanyonge wanaotengwa kinyume cha fikra za Mungu za huruma kama tulivyosikia jumapili iliyopita juu ya Msamaria mwema. Baada ya kupambana na nguvu hizo, Yesu amechoka, anahitaji kukaribishwa kwenye nyumba ya familia yoyote ile aweze kutuliza mapigo ya moyo kidogo. Kitendo cha Mungu kutaka kutulia chaonesha jinsi anavyoguswa na mahangaiko ya binadamu, anaowatakia pia kupumzika. Chaonesha pia mwamba hata Yesu anahitaji urafiki wetu na kukaribishwa na kwamba anavijali na anataka kuviinjilisha vionjo vya binadamu. Kwa mtazamo huo tuone sasa jinsi mambo yalivyo katika fasuli ya leo. “Ikawa katika kuenenda kwao aliingia katika kijiji kimoja; mwanamke mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake.” Ujumbe wa kwanza wa fasuli hii unaupata katika neno hili kukaribisha. Mungu anapenda kukaribishwa na hivi nyumba yetu ni roho zetu na Yesu ni kama Bwana arusi anayesema: “Mimi niko mlangoni ninagonga, anayetaka kunipokea nitaingia kwake na kufanya makao yangu kwake.” (Ufu 3). Hapa Yesu anabadili utamaduni wa taifa lake, kwani wakati wake, haikuwezekana kwa mwamume kukubali mwaliko wa  mwanamke.

Aidha yasemwa kwamba, “Dada yake aitwaye Mariamu, aliketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno yake.” Katika nyumba ya Mpalestina hakukuwa na viti bali kulikuwa na vigoda, na Maria aliketi chini miguuni pa Yesu. Mkao wa Maria ulikuwa wa wanafunzi wanapomsikiliza mwalimu kama anavyosema Paulo: “Mimi nilikuwa nimeketi katika miguu ya Gamalieli, yaani nilikuwa mwanafunzi wake.” Kwa hiyo Maria alikuwa mwanafunzi anayemsikiliza Yesu. Katika utamaduni wa Wayaudi rabi (mwalimu) hakuweza kamwe kumruhusu mwanamke kuketi miguuni pake. Kuna semi kadhaa zinazomharamisha mwanamke kufanya mambo ya kidini, Kwa mfano walisema: “ni afadhali kuunguza Biblia kuliko kumpa mwanamke,” au “Mwanamke asithubutu kubariki chakula,” au “Mwanamke akienda kwenye Sinagogi, huko ajifiche asijitokeze kamdasi.” Fikra hizi ziliathiri pia jumuiya ya kwanza ya wakristu, kama vile ile miongozo aliyotoa Paolo kwa Wakorinto: “ni marufuku wanawake kuongea kwenye halaiki ya watu. Kama mwanamke anataka kusema kitu fulani kihusucho Maandiko Matakatifu basi akamwulize mume wake.” Kwa hiyo Injili ya Yesu inafuta ubaguzi wa jinsia.

Kuhusu Maria kukaa pale miguuni pa Yesu, wengine wanamfasiri kuwa kama ni kioo cha watawa wa maisha ya taamuli yanayoitwa contemplative life, tofauti na Martha anayeishi maisha ya vitendo wanayoita active life. Tafsiri hii inapotosha kabisa maana ya Injili hii. Hapa fasuli imesema waziwazi kwamba “Mariamu aliketi miguuni pa Yesu, akasikiliza maneno yake.” Dada huyu alikuwa anasikiliza Neno la Yesu hakukaa pale kufanya sala ya taamuli, na kuhusu Martha imesemwa waziwazi kuwa “alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi.” Hivi hapa kuna kusikiliza na kuhangaika. Tatizo la Martha lilikuwa ni kuhaha.

Kwa maneno mengine, kwake yeye ilikuwa “Hapa kazi tu hadi kieleweke.” Kwa mantiki hiyo Martha ni picha halisi ya wachapa kazi tena zile muhimu zenye tija katika maisha, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Martha analinganishwa na wale wanaotia mzigo wa kazi maofisini, mashambani, masokoni tangu asubuhi sana hadi jioni sana, wakirudi nyumbani ni choka mbaya!. Wanazo simu za mkononi zaidi ya tano na kila moja inaita kwa mfululizo na picha kuingia mara kwa mara utadhani unaangalia filamu.

Wana Ipad kadhaa zinazoingiza sms mbalimbali za kikazi na kijami hata wakati mwingine ni burudani kwenda mbele. Kama ni Padre au Askofu, anaweza kuingia kwenye kitubio, au kwenye misa na simu mbili au tatu zimetegwa katika ”vaibresheni”. Anashughulika na vijana, anaenda kwa vikundi vya Legio Maria na kutembelea Jumuia ndogondogo, nk. Hadi inapofika jioni mtu huyo yuko hoi bin taabani. Siku ya pili anaendelea tena na shughulika kama jana hakuna cha jumamosi wala jumapili. Ukimwuliza malengo na makusudio ya mihangaiko hii yote, atakujibu: “Hapa kazi tu.” Ni vyema na vizuri kwamba amejikita katika mambo muhimu na yenye mapato mazuri. Lakini mtu huyu anashindwa kujihoji, anavyoishi na mwisho na ni nini hatima ya maisha yake. Ndivyo ilivyokuwa kwa dada yetu Martha. Alizama katika shughuli muhimu kabisa za kuandaa chakula akakosa hata muda wa kupumua. Hakutulia hakuwa na raha na hakujihoji alikuwa anaishi nini na anaenda wapi.

Watu wanaohaha na kufanya kazi kama Martha, hawana furaha, kwani hawana bado mwono wazi wa kitu wanachofanya. Hawatulii, hawana amani na hawaridhiki. Aidha utawagundua kirahisi sana kutoka nje jinsi walivyokaa kiugomvi ugomvi, kwa kukasirika-kasirika na kuhangaika. Kwao, kila siku ni mbaya, wanabaki kukosoa kila kitu wanachofanya wengine. Kuonesha kwamba Martha alikuwa na tabia hizi unamwona jinsi anavyohaha. Badala ya kwenda kumwomba dada yake amsaidie kazi, yeye anaenda kumvaa mgeni Yesu na kumwuliza swali la kumchoma dhamiri: “Bwana huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie anisaidie.” Ni dhahiri dada huyu alikuwa anafanya kazi muhimu sana lakini unamwona wazi kwamba hajaingia ndani kwenye kiini cha lengo la kazi anayofanya ndiyo maana ameanza mapambano ya maneno.

Kumbe, endapo Martha angeifanya kazi yake baada ya kulisikiliza kwanza Neno, angejua wazi jinsi ya kufanya kazi yake na kuiipa thamani ya maisha na angetambua maana ya kazi yake. Hadi hapa Yesu anaona amwinjilishe anamtolea uvivu. Hivi anamwita ili kumpa mwito mpya na namna itakiwayo ya kutawala vionjo vya kazi. “Martha, Martha.” Katika Biblia ukiitwa jina mara mbili, ujue huo ni mwito maalumu na kuna jambo zito: Mathalani “Samweli, Samweli!” “Musa, Musa!”, “Abraham, Abraham!” “Sauli, Sauli!” Martha anatajwa mara mbili na kuambiwa “unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi” Neno hili unasumbuka kwa kigiriki ni merimnas maana yake ni kuhaha ndani ya moyo. Kwamba anajibamiza katika kazi bila kutafakari lengo linalounganisha kazi anayofanya.

Hivi ndivyo inavyokuwa kwa watu wanaohangaika katika maisha, hata kama wanafanikiwa lakini jambo walifanyalo halina mlengo mkuu wa maisha yao. Martha anawakilisha wale wanaohaha na maisha haya lakini siyo maisha yaliyoungana na mapenzi ya Mungu. Yesu anaendelea kusema: “Lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Maria amelichangua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.” Tafsiri ya fungu lililo jema, imepotoshwa sana kwani kwa Mungu hakuna fungu jema wala fungu baya. Kutokana na tafsiri hii ya fungu jema, Papa Gregori mkuu alitofautisha ngazi tatu za utakatifu: Ngazi ya chini ya utakatifu ni ya walei. Ngazi ya kati ni ya makuhani (mapadre), na ngazi ya juu kabisa ya utakatifu kama ule wa Mama Maria ndiyo maisha ya wamonaki au watawa, yaani maisha ya taamuli.

Kumbe, Yesu hazungumzii juu ya ngazi hizi za utakatifu, bali “fungu lililo jema,” yaani ili uweze kupata maana ya halisi ya maisha, kabla ya kutenda jambo lolote “yatakiwa kitu kimoja tu ” nacho ni kuketi miguuni pa Yesu na kulisikiliza Neno. Maana yake unatakiwa upate nadharia kabla ya vitendo na mtoa nadharia hiyo ni Yesu mwenyewe.

Baada ya majibu ya Yesu tungetegemea Martha angedakiza tena, kumbe, lakini anafumba mdomo na kukaa kimya. Kwamba, baada ya kusikiliza maneno ya Yesu sasa aliweza kurudi jikoni kuendelea na kazi akiwa sasa anatambua lengo muhimu la kufanya kazi, ambalo ni kutumikia kwa upendo na kwa furaha bila kuhaha wala kuwatupia wengine madongo kana kwamba, umeambiwa kuwasaidia kufanya kazi. Kwa upande wa Maria, si haba kama kiatu cha raba! Naye hasemi kitu, lakini kutoka kwake tunaweza kupata fundisho hasa kutokana na vituko alivyofanya alipokuwa Betania katika Injili ya Yohane yasemwa: “Basi Mariamu akatwaa ratli ya marhamu ya nardo safi yenye thamani nyingi akampaka Yesu miguu, akamfuta miguu kwa nywele zake. Nayo nyumba pia ikajaa harufu ya marhamu.” (Yoh 12: 3). Mafuta ni alama ya upendo na kumpaka miguu ya Yesu ni alama ya utumishi wa upendo utolewao bure bila masharti kwa mwenye dhiki.

Hivi ndivyo afanyavyo Maria baada ya kuelewa maana ya maisha sasa anafanya yote kwa ajili ya mapendo kamili pasi na shuruti wala ndoana! Kwani kuna mapendo mengine waswahili wanasema nipe nikupe! Haya ni mapendo ya ndoana, ukimeza utakiona che mtema kuni! Ndugu yangu haya ndiyo mapendekezo tunayopata leo. Yesu halaani kazi ya Martha, bali anataka kutupatia ushauri nasahaa kuwa: “Tuwe makini na kazi tuzifanyazo kwani zaweza kutuletea vurugu mtupu kama hutuzipatii maana ya maisha. Na maana hiyo unaipata tu katika kulisikiliza Neno  lake." Yesu anatuambia “Tuwasiliane kabla hamjatenda kazi ili kuyapatia maana maisha yenu.”

Na Padre Alcuin Nyirenda, OSB.








All the contents on this site are copyrighted ©.