2016-07-15 15:02:00

Huruma ya Mungu imefumbatwa katika Neno lake!


Mwaka wa Jubilei ya Huruma ya Mungu umetuletea daima masikioni mwetu mwaliko wa kuikimbilia huruma ya Mungu na kuwa wajumbe wake kwa kuifanya ionjwe na binadamu wote. Wajibu huu ambao ni muhtasari wa wito wetu wa kikristo wa kwenda kuitangaza habari njema ya wokovu kwa watu wote unatudai mambo mawili muhimu ambayo bila hayo tutaishia katika utumishi usiokuwa na matunda yanayotarajiwa. Mambo hayo ni kujiweka chini ya Kristo na kulisikiliza Neno lake. Utajiri wa Mungu umefichika katika Neno lake na hivyo usikivu wetu kwa Neno hilo linalojifunua kwetu kwa namna ya pekee kwa njia ya Kristo ndio njia ya kutupatia majibu chanya. Katika Dominika hii ya 16 ya Mwaka wa Kanisa Neno la Mungu linatufafanulia wajibu huu na majibu chanya yatokanayo nalo.

“Naye alikuwa na umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno yake”. Kifungu hiki cha Biblia ndicho kitatuongoza katika kujitafakari na kuzitengeneza njia zetu ili kutimiza vema wajibu wetu kwa Mungu na kwa jirani zetu. Utumishi wetu unatututaka kwanza kujiweka chini ya Kristo. Huku kunajionesha katika kulisikiliza Neno lake na kuyashika mafundisho yake. Fadhila kuu tatu za kimungu zinadokezwa hapa. Kwanza ni imani kwa Mungu, paji ambalo linatuhakikishia yale yote yaliyoahidiwa na hata yale tusiyoweza kuyaona. Tutaweza kukaa chini yake na kulisikiliza neno lake kwa sababu tunayo imani kwake.

Pili ni matumaini. Yeye ambaye yu tayari kujiweka chini ya Mungu na kulisikiliza Neno lake yu mithili ya mtoto mchanga mikononi mwa mama yake. Anatumaini kutimiziwa mahitaji yake yote ya muhimu na hivyo hana shaka na jambo lolote. Tatu ni upendo. Upendo wetu kwa Mungu unatufanya kujikabidhisha kwake wazima wazima bila kujibakisha kwa vingine au wengine, bila kuangalia nyuma kwamba unaacha nini au bila kuangalia pembeni kwamba wengine wanafanya nini au wanaangalia nini.

Ujumbe wa Kristo wakati mwingine unapingana na matakwa ya ulimwengu wetu lakini sisi kama wajumbe wake hatupaswi kuyumbishwa na hilo. Mtume Paulo katika somo la pili anatupatia picha halisi ya utumishi huo unaojikita katika Kristo ambao kwa sababu ya upinzani wa ulimwengu huu hauwezi kamwe kuepa kupitia njia ya mateso. Anatueleza kuwa katika mazingira hayo ya msalaba, yaani mateso amewekwa kuwa mtumishi wa kuifunua siri ya utukukufu wa Mungu kwa mataifa ambayo ni Kristo mwenyewe. Hivyo fadhila kuu tatu za kimungu nilizozidokeza hapo juu zinatusukuma katika kujiweka chini ya miguu ya Kristo na kumsikiliza, yaani kuwa wakati wote kutenda, kusema na hata kuwaza kadiri ya Neno lake bila kujali makandokando ya ulimwengu. Ni pale tu tutakapokuwa tayari kujimithilisha na msalaba wa Kristo ndipo tutakapoweza kusonga mbele katika utumishi wetu.

Kujiweka chini ya miguu ya Kristo na kumsikiliza inatudai sisi kutumikia katika ukamilifu wote bila kuangalia tutapata nini au bila kuangalia wenzangu wanafanya nini. Mara nyingi tunajikuta tupo katika kishawishi kama cha Martha. Tunaambatanisha utumishi wetu na lawama kwa wengine ambao hawatendi kama unavyotenda. Hii inadhihirisha kwamba utendaji wako si kwa ajili ya kuufunua utukufu wa Mungu na kumdhihirisha Kristo bali ni katika kutafuta kuonekana, kupata jina na umaarufu. Wakati mwingie tunashuhudia sisi wenyewe tukianza kulalamika pale tuonapo kazi zetu hazithaminiwi na wengine au pengine kudhani kwamba wengine wanategea katika kutimiza wajibu fulani. Kwa nafasi nyingine tunajikuta tupo katika nafasi ya kunung’unika kwa kupokea ujira kidogo au malipo kidogo kutokana na ukarimu au kazi tunayotenda bila hata kujali hali halisi ya unayemdai. Huduma yetu inageuka ni njia ya unyonyaji  na si sababu ya kuwafanya wengine waionje huruma ya Mungu.

Kristo aliposema kwamba “Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa” haikumaanisha kwamba hakuthamini huduma ya ukarimu ailiyokuwa ikitolewa na Martha. Fundisho la Kristo kwetu ni kwamba, matendo yetu ya huruma yasipojikita katika kukaa miguuni kwake kumsikiliza yataashia tu kuwa ni fadhaa na mahangaiko. Yatatufanya tusiwe na amani na utume wetu tunaoutekeleza. Pengine mimi na wewe tumekuwa katika kundi hilo. Maneno ya Kristo kwa Martha yanatujia nasi leo hii akisema “unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa”.

Katika somo la kwanza Baba yetu wa imani Ibrahimu anatupatia mfano wa kuwapokea wageni na kuwakirimia na matokeo yake anaahidiwa uzao, jambo ambalo alilitamani katika maisha yake yote hadi alipofikia uzee. Upendo wake kwa watu hawa wanamtembelea unasukumwa na imani yake thabiti kwa Mungu. Kwake yeye haijalishi kwamba yupo katika hali ya uzee, kwamba hana mtoto kwa mkewe Sara jambo ambalo lineweza kumuondoa katika hali ya kuangalia wengine. Tangu mwanzoni amekuwa mtu wa imani kuu kwa Mungu, daima alijiweka chini ya miguu ya Mungu na kumsikiliza na hivyo imani yake hii inamsukuma kutenda kwa upendo: “nami nitaleta chakula kidogo, mkaburudishe moyo, baadaye mwendelee, iwapo mmemjia mtumwa wenu”. Yeye kama asemavyo mzaburi “hakutoa fedha ili apate kula riba bali huwaheshimu wamchao Bwana”. Mwisho mwa yote anajibiwa hamu ya moyo wake: “hakika nitakurudia wakati uu huu mwakani, Sara mkeo atapata mtoto wa kiume”. Yote haya yalitimia kwake kwa sababu alijiweka chini ya miguu ya Mungu na kulisikiliza neno lake alipomwahidi akisema “tazama mbinguni, kazihesabu nyota, kama ukiweza kuzihesabu ... ndivyo utakavyokuwa uzao wako” (Mw 15:5).

Kristo anatujia leo hii kwa namna mbalimbali akihitaji kila mmoja wetu kwa nafasi yake kujiweka chini ya miguu yake na kumsikiliza. Leo hii tunaangaika kutenda mengi kwa wengine kwa ajili ya kuwapatia faraja na nafasi ya kuionja huruma ya Mungu. Matendo hayo yanaweza kujumuishwa katika kazi za huruma ya Mungu tulizoelekezwa na Baba Mtakatifu wakati huu wa Jubilei ya huruma ya Mungu: kuwalisha wenye njaa, kuwanywesha wenye kiu, kuwahifadhi wageni, kuwavisha walio uchi, kuwafariji wagonjwa, kuwatembelea wafungwa na kuwazika wafu. Lakini matendo haya yanaweza kugeuka kwetu kuwa fadhaa na mahangaiko kama hatutajiweka chini ya Kristo na kumsikiliza. Tunasukumwa kuasisi matendo mbalimbali ya huruma lakini aghalabu kudhihirisha kama kweli tupo chini ya Kristo na tunamsikiliza. Tunafanya huduma mbalimbali lakini si katika ukweli bali ni katika kujipanua zaidi sifa zetu na pale inapoonekana hiyo nia yetu kuathirika basi matendo hayo hata kama huleta faraja kwa wengine kwetu huwa ni maangaiko na huzuni.

“Mariamu amelichagua fungu jema, ambalo hataondolewa”. Huo ndiyo wito wa Kristo kwetu leo hii. Tuombe katika Dominika hii neema ya Mungu ili ituwezeshe kudumu katika kulisikiliza Neno lake linalofunuliwa kwetu kwa njia ya Kristo kusudi Neno hilo liimarishe imani na upendo wetu na hivyo kuwa kweli mawakili wema wa huruma ya Mungu kwanza kwetu sisi wenyewe na kwa wengine.

Kutoka studio za Radio Vatican mimi ni Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.