2016-07-14 14:38:00

Moto wa Uinjilishaji mpya nchini Ufilippini!


Kardinali Luis Antonio Tagle, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila nchini Ufilippini anasema, Kongamano la tatu la Uinjilishaji mpya nchini Ufilippini litakaloanza kutumia vumbi kuanzia tarehe 15 – 17 Julai 2016 utakuwa ni moto wa kuotea mbali kwani familia ya Mungu nchini Ufilippini itakuwa inawasha moto wa Injili ya huruma ya Mungu katika nyoyo za watu kwa kujikita katika maneno makuu matatu kutoka Ufilippini yaani: “Awa”, “Unawa”, “Gawa” kwa lugha ya Kiswahili ni “Huruma”, “Uelewa” na “Upendo”.

Maadhimisho ya Kongamano hili yatafunguliwa kwa Ibada ya Misa takatifu itakayoongozwa na Kardinali Tagle na baadaye wajumbe pia watashiriki katika tafakari juu ya “Wamissionari wa huruma ya Mungu”. Hawa ni Mapadre walioteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kwenda sehemu mbali mbali za dunia ili kuwaondolea watu dhambi ambazo kimsingi zinaondolewa tu na Kiti kitakatifu, ili kweli familia ya Mungu iweze kuguswa na kuonja huruma na upendo wa Mungu wakati huu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu.

Kashfa ya huruma ya Mungu ni tema inayosubiriwa na wengi kwa hamu kubwa kwa sababu haki ya Mungu ni huruma yake. Hii itakuwa ni fursa makini ya kuweza kuchambua huruma na upendo wa Mungu kama unavyooneshwa na Kristo Yesu katika mfano wa Baba mwenye huruma aliyemwonea huruma kijana wake mdogo aliyekuwa amechomoka na “vigunia” vya fedha ya urithi na kuzitapanya huko kwa maisha ya anasa na starehe.

Kongamano hili litakuwa ni fursa ya shuhuda za matendo ya huruma: kiroho na kimwili wakati huu Mama Kanisa anapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, baada ya kusikiliza tafakari ya kina kuhusu uelewa wa huruma ya Mungu kadiri ya elimu ya binadamu. Askofu mkuu Giuseppe Pinto, Balozi wa Vatican nchini Ufilippini atakunja jamvi la kongamano la tatu la Uinjilishaji mpya nchini Ufilippini kwa Ibada ya Misa takatifu.

Kardinali Tagle anakaza kusema, ulimwengu mamboleo una kiu na njaa ya huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha ushuhuda wa imani tendaji. Mchakato wa Uinjilishaji hauna budi kufumbatwa na shuhuda za umwilishaji wa huruma ya Mungu katika uhalisia wa maisha ya binadamu, ili kweli maisha ya binadamu yaguswe na huruma hii. Katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na matukio ya kigaidi ambayo yamewagusa na kuwatikisa watu wengi duniani. Matukio haya yanaonesha kwamba, walimwengu kweli wana kiu na njaa ya huruma ya Mungu.

Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 2013 kwa mara ya kwanza nchini Ufilippini kuliadhimishwa Kongamano la Uinjilishaji mpya. Baba Mtakatifu Francisko akawatumia ujumbe kwa njia ya video huku akiwataka waamini nchini Ufilippini kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wasaidie mchakato wa kumpeleka Kristo Yesu katika medani mbali mbali za maisha sanjari na kujikita katika dhana ya utamadunisho, ili kweli tunu msingi za Kiinjili ziweze kukita mizizi yake katika maisha na vipaumbele vya watu, bila kusahau kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Papa Francisko aliitaka familia ya Mungu nchini humo kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya waananchi wa Ufilippini na Bara la Asia katika ujumla wake. Kongamano la Pili la Uinjilishaji mpya liliadhimishwa Jijini Pasay kunako mwaka 2015.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.