2016-07-14 15:04:00

Michezo kwa ajili ya huduma kwa binadamu!


Baraza la Kipapa la Utamaduni linaendelea kuwekeza katika michezo kama sehemu muhimu sana ya huduma kwa binadamu. Kuanzia tarehe 5 - 7 Oktoba, 2016, kutafanayika mkutano wa kimataifa utakaowashirikisha viongozi 150. Lengo ni kujadili kwa kina na mapana kuhusu ushirikiano wa karibu kati ya imani na michezo ili kuboresha maisha ya watu wengi zaidi kwa kuongozwa na kanuni sita msingi. Mkutano huu utawashirikisha viongozi wa michezo, wafabiashara na viongozi wa kijamii ili kuibua kanuni msingi zitakazotumika kuongoza kikundi hiki.

Kardinali Gianfranco Ravasi Rais wa Baraza la Kipapa la Utamaduni anasema Baraza lake limekubali “Allianz” kuwa ni muasisi mfadhili wa  mkutano wa kimataifa wa michezo kwa ajili ya huduma kwa binadamu. Changamoto ya michezo kwa ajili ya huduma ya michezo kwa binadamu ilitolewa na Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni anayewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuchukulia changamoto ya maisha kama michezo. Lengo ni kuboresha maisha ya binadamu katika medani mbali mbali.

Kwa upande wake Bwana Oliver Bate, Mkurugenzi mkuu wa “Allianz” anasema, wanaona kwamba, wamepewa heshima kubwa na Baraza la Kipapa la Utamaduni kuzindua kikundi hiki kitakachowasaidia watu kuishi kwa ujasiri sanjari na kuendelea kujenga madaraja ya watu kukutana tayari kufanya mageuzi makubwa katika maisha na vipaumbele vyao. "Allianz" Itasaidia timu za michezo kwa kuwahamasisha vijana kushiriki katika mbinu mkakati zinazotolewa na kikundi hiki kwa kuonesha kwamba, wanaweza kuchangia katika masuala ya michezo na maisha katika ujumla wake.

Monsinyo Melchior Sanchez de Toca, Katibu mkuu msaidizi, Baraza la Kipapa la Utamaduni anasema kwamba, hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Vatican kufanya mkutano wa ngazi ya juu kuhusu masuala ya imani na michezo. Tukio hili si moto wa mabua, bali linapania kujenga ushirikiano kati ya watu wa imani, dini, tamaduni na maeneo tofauti ya kijiografia. Baraza la Kipapa la Utamaduni linaendelea kushughulikia mialiko ili viongozi wengi zaidi waweze kushiriki katika mkutano huu. Kati ya viongozi maarufu ni Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-Moon na Bwana Thomas Bach, Mwenyekiti wa Kamati ya Olympic Kimataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.