2016-07-14 09:26:00

Majadiliano ya kidini yanapania kujenga: haki, amani na maridhiano!


Askofu Miguel Angel Ayuso Guixot, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini akiwa ameongozana na Askofu mkuu Bruno Musarò, Balozi wa Vatican nchini Misri, Jumatano, tarehe 13 Julai 2016 wamekutana na kuzungumza na Dr. Kamal Abd al Salam, mjumbe wa Kituo cha Majadiliano ya kidini cha Al – Azhar akiwa ameandamana na Dr. Zakzouk pamoja na Prof. Mohey El Din Afifi Ahmed, Katibu mkuu wa Kituo cha Utafiti cha Kiislam cha Al- Azhar.

Ujumbe wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini, baadaye umekutana na kuzungumza pia na Dr. Abbas Shouman  Wakili wa Al - Azhar. Mazungumzo haya yamekuwa na mafanikio makubwa kadiri ya taarifa iliyotolewa na Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini. Askofu Guixot amewasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na kujadiliana mambo msingi ambayo yanapaswa kupewa kipaumbele cha pekee wakati wa majadiliano kati ya Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini na Chuo kikuu cha Al - Azhar cha Cairo, nchini Misri.

Baba Mtakatifu Francisko alikuwa amelihamasisha Baraza la Kipapa la majadiliano ya kidini kuhakikisha kwamba, linafufua tena majadiliano na Chuo kikuu cha Al – Azhar cha Cairo. Mazungumzo baina ya viongozi hawa yamefanyika katika hali ya utulivu na amani, kwa kuonesha umuhimu wa majadiliano ya kidini yanayojikita katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi sanjari na kuimarisha mahusiano mema kati ya waamini wa dini ya Kiislam na Kikristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP. S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.