2016-07-14 15:23:00

Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi duniani!


Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa: Missio, Focsiv na Caritas, yamehitimisha semina ya kimataifa iliyokuwa inapembua kwa kina na mapana kuhusu mpasuko wa Umoja wa Ulaya pamoja na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta usalama na hifadhi ya maisha Barani Ulaya. Wengi wa wakimbizi na wahamiaji hawa kwa sasa wanapata hifadhi nchini Ugiriki ambayo kwa sasa inakabiliana na mtikisiko wa uchumi kimataifa ambao kwa muda wa miaka sita umesababisha madhara makubwa kwa maisha ya watu, kiasi hata cha kuwakatisha tamaa.

Tangu mwaka 2015 zaidi ya wakimbizi na wahamiaji million moja wamepita na kuvuta mipaka ya Ugiriki huku wakitafuta usalama na hifadhi ya maisha Barani Ulaya kutoka katika nchi zenye vita, nyanyaso, madhulumu ya kidini, umaskini na majanga asilia. Wajumbe wamepata fursa ya kupembu kwa umakini mkubwa hali ya wakimbizi kitaifa na kimataifa pamoja na kushirikishana uzoefu na mang’amuzi kutoka kwa Makanisa mahalia jinsi ambavyo yanaendelea kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji licha ya hali ngumu ya maisha, kielelezo cha mshikamano wa dhati hata katika umaskini na hali ngumu ya maisha.

Hapa utu na heshima ya binadamu ndivyo vinavyopewa kipaumbele cha kwanza, ili kuokoa maisha ambayo kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Imekuwa ni nafasi ya kuibua mbinu mkakati wa ujenzi wa madaraja ya upendo na mshikamano Barani Ulaya kwa ajili ya kuendelea kuwasaidia na kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji.

Wajumbe wanautaka Umoja wa Ulaya kujikita katika utawala wa sheria, haki msingi za binadamu, mshikamano, ukarimu pamoja na kuendeleza mchakato wa kuwaingiza wakimbizi na wahamiaji katika sera na mikakati ya nchi wanachama kuliko mwelekeo wa sasa unaojionesha kwa kutaka kujenga kuta za utengano na ubaguzi dhidi ya wakimbizi na wahamiaji wanaotaka hifadhi na usalama wa maisha Barani Ulaya.

Wajumbe wa semina hii ya kimataifa katika tamko lao wanapenda kurejea kwenye maneno ya Baba Mtakatifu Francisko kwa kusema kwamba, ikiwa kama Bara la Ulaya linataka kuambata mchakato wa ujenzi wa familia kubwa ya binadamu, halina budi kwanza kabisa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu, kwa kuonesha upendo, ukarimu na mshikamano si tu katika masuala ya kiuchumi bali hata katika mambo ya kijamii na kitamaduni.

Wajumbe wanasema, wanaendelea kuendesha kampeni kwa kuwataka wakimbizi na wahamiaji kutekeleza haki ya kubaki katika nchi zao kama sehemu ya ujenzi wa umoja wa familia kubwa ya binadamu sanjari na kuhakikisha kwamba, watu wengi zaidi wanakuwa na uhakika wa usalama wa chakula duniani. Hii ni dhamana inayotekelezwa na Mama Kanisa kwa njia ya Mashirika ya misaada ya Kanisa Katoliki kitaifa na kimataifa. Umoja wa Ulaya na nchi wanachama wake waguswe na mahangaiko ya wananchi wa Ugiriki na Ulaya katika ujumla wake kwa kuanza kujifunga kibwebwe ili kupambana na umaskini wa hali na kipato pamoja na uratibu na huduma kwa wimbi la wakimbizi na wahamiaji duniani.

Wajumbe wanaziomba Serikali pamoja na taasisi zake kuibua mbinu mkakati utakaosaidia mchakato wa kukuza na kuendeleza maendeleo endelevu kwa kujikita katika mshikamao unaoongozwa na kanuni auni kama mambo msingi yanayoweza kulisaidia Bara la Ulaya kupita kipindi hiki kigumu cha historia ya uwepo wake: Ugiriki inahitaji kupewa mwelekeo mpya wa misaada pamoja na kusaidia nchi ambazo kwa sasa zinakabaliwa na hali ngumu ya uchumi kutokana na mtikisiko wa uchumi kitaifa na kimataifa, kwa kuwekeza zaidi kwa fursa za ajira miongoni mwa vijana ili kuwajengea matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi.

Hapa kuna haja ya kusimama kidete kupinga sera za ubaguzi na ukosefu wa usawa na haki msingi za binadamu; Ukosefu wa usalama, fursa za ajira na maisha ya binadamu pamoja na ujenzi wa kuta dhidi ya wakimbizi na wahamiaji wanaotaka hifadhi na usalama wa maisha yao Barani Ulaya. Ujenzi wa kuta na uwepo mkubwa wa vyombo vya ulinzi na usalama mipakani si suluhu ya kuweza kudhibiti wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta hifadhi na usalama wa maisha Barani Ulaya.

Umoja wa Ulaya ushirikiane na Umoja wa Mataifa ili kuweza kupata suluhu ya changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kwa wakati huu. Kuna haja pia ya kuwekeza katika sera na mikakati ya ushirikiano wa kimataifa; haki, amani na maridhiano kati ya watu ili kuondokana na vita, mipasuko pamoja na kinzani za kijamii ambazo zimekuwa ni chanzo kikuu cha wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani.

Bara la Ulaya lililogawanyika litatumbukia katika dimbwi la umaskini kwa kuelemewa na udhaifu pamoja na uzee. Bara la Ulaya liloungana na kushikamana litaweza kudumisha misingi ya usawa, litakuwa na utajiri mkubwa na lenye nguvu na daima litakuwa linajisimika katika ujana na kwamba, mwelekeo wa namna hii utausaidia hata Umoja wa Ulaya kuratibu na kuwahudumia vyema wakimbizi na wahamiaji wanaotaka maisha bora zaidi Barani Ulaya. Kofi Annan aliwahi kusema, Umoja wa Ulaya unapaswa kuonesha mshikamano wa dhati ndani na nje ya mipaka yake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican. 








All the contents on this site are copyrighted ©.