2016-07-14 07:12:00

Askofu mkuu Zimowski: Shuhuda wa imani katika ugonjwa!


Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, Rais wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya aliyefariki dunia akiwa kwenye hospitali ya Dabrowa Tarnowska, nchini Poland usiku wa kuamkia tarehe 13 Julai 2016, akiwa na umri wa miaka 67.

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa Monsinyo Jean-Marie Mate Musivi Mupendawatu, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya anasema, Askofu mkuu Zimowski ameugua kwa muda mrefu na akafanikiwa kupokea mateso na mahangaiko yake kwa imani na ushuhuda wa Kikristo. Baba Mtakatifu anapenda kuungana kiroho na Baraza Kipapa la huduma za kichungaji kwa wafanyakazi katika sekta ya afya wakati huu wanapoomboleza kifo cha Askofu mkuu Zimowski.

Baba Mtakatifu anamkumbuka kwa namna ya pekee katika huduma makini za kichungaji alizotoa alipokuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Radom, Poland na baadaye alipoteuliwa kutoa huduma yake mjini Vatican. Baba Mtakatifu anapenda kutoa sala zake kwa ajili ya kuombea roho ya Marehemu Askofu mkuu Zimowski, akiiweka chini ya maombezi ya Bikira Maria, Malkia wa Poland.

Baba Mtakatifu anaungana na wafanyakazi wote, ndugu na jamaa kwa ajili ya kumwombea Marehemu Askofu mkuu Zimowski maisha ya uzima wa milele yaliyoandaliwa kwa wahudumu waaminifu wa Injili. Mwishoni, Baba Mtakatifu anapenda kutoa baraka zake za kitume kwa wote walioguswa na msiba huu mzito! Taarifa zinasema, kwamba, hivi karibuni, Baba Mtakatifu Francisko aliwasiliana na Askofu mkuu Zimowski alipokuwa amelazwa na kumtakia nafuu katika ugonjwa wa Saratani ya ini ambao uligunduliwa kunako mwaka 2014. Baba Mtakatifu mstaafu Benedikto XVI aliwasiliana naye pia kwa njia ya simu.

Hayati Askofu mkuu Zygmunt Zimowski alikuwa ni mtaalam wa hati ya Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu “Fumbo la Kanisa” “Lumen Gentium”. Kunako tarehe 1 Februari 1983 alianza kutoa huduma yake ya kitume kwenye Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa, wakati huo chini ya Kardinali Joseph Ratzinger. Alishiriki kikamilifu katika kuandaa Katekisimu Mpya ya Kanisa Katoliki kwa lugha ya Kipolandi. Itakumbukwa kwamba, Katekisimu ni muhtasari wa: Imani, Sakramenti, Maisha na Sala za Kanisa.

Itakumbukwa kwamba, Mwezi Desemba 2014, Askofu mkuu Zimowski alilazwa huko Varsavia na kugundulika kwamba, alikuwa anasumbuliwa na Saratani ya ini. Tarehe 8 Februari 2015 kama sehemu ya maandalizi ya Siku ya Wagonjwa Duniani, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican alimkumbuka na kuwaomba waamini kumsindikiza kwa sala na sadaka zao.

Mwezi Mei, 2015 akarejea mjini Vatican kuendelea na utume wake miongoni mwa wagonjwa. Kwa mara ya mwisho, aliweza kuonekana hadharani tarehe 11 Februari 2016 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Wagonjwa Duniani, ambayo kwa mwaka huu, iliadhimishwa mjini Nazareti, Nchi takatifu. Tangu wakati wa maadhimisho ya Siku kuu ya Pasaka kwa mwaka 2016, Askofu mkuu Zygmunt Zimowski alirejea nchini Poland ili kuendelea na matibabu yake kwa imani na matumaini. Marehemu Askofu mkuu Zimowski, atalazwa kwenye nyumba ya milele akiwa na tumaini la ufufuko hapo tarehe 19 Julai 2016, Jimboni Radom, nchini Poland. RIP.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.