2016-07-13 07:59:00

Ujumbe wa matumaini kwa familia ya Mungu Sudan ya Kusini


Baraza la Makanisa Kusini mwa Sudan linasikitishwa sana na vita iliyofumuka tena nchini humo na kusababisha mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, uharibifu mkubwa wa mali pamoja na kupelekea watu wengi kuyakimbia makazi yao, ili kusalimisha maisha yao. Mapigano haya yameanza kutimua vumbi hapo tarehe 7 Julai 2016, siku ambapo Sudan ya Kusini ilikuwa inapaswa kuadhimisha kumbu kumbu ya miaka 5 tangu iliyopojipatia uhuru wake, lakini maadhimisho haya yamegeuka kuwa ni uwanja wa vita, kinzani na mipasuko ya kisiasa.

Familia ya Mungu Kusini mwa Sudan baada ya vita ya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka miwili, ilidhani kwamba, mkataba ya wamani uliotiwa sahihi kunako mwaka 2015 na hivyo kuanza mchakato wa kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa, ungekuwa ni mwanzo wa amani, lakini bado wananchi wanateseka kutokana na vita isiyokuwa na mashiko wala mvuto kwa wananchi wengi wa Sudan ya Kusini.  Baraza la Makanisa nchini Sudan ya Kusini linawataka wanajeshi wa Serikali pamoja na wale wa upinzani kuweka silaha zao chini ili kusalimisha maisha ya wananchi.

Viongozi wa Makanisa wanasema, jambo la msingi kwa wakati huu ni kuokoa maisha ya wananchi kwa kusitisha mapigano na kwamba, kuna haja ya kufanya majadiliano katika ukweli na uwazi kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Sudan ya Kusini. Katika siku za hivi karibuni kumekuwepo na shutuma kutoka kwa kila upande kuhusu uvunjifu wa mkataba wa amani. Wakati wa vita na mapigano umekwisha, sasa viongozi wa kisiasa wanapaswa kujifunga kibwebwe kujenga na kudumisha Sudan ya Kusini inayosimikwa katika misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Viongozi wa Makanisa wanashukuru kwa tamko la viongozi wa Serikali na upinzani wa kusitisha mapigano, lakini pia kuna mauaji ya watu wasiokuwa na hatia yanaendelea kufanyika nje ya mji mkuu wa Juba, Sudan ya Kusini. Viongozi wa Makanisa wanahitimisha ujumbe wao kwa kuombea amani na matumaini kwa Sudan ya Kusini.

Wakati huo huo, Maaskofu Katoliki Kusini mwa Sudan katika maadhimisho ya Miaka 5 ya Uhuru wa Sudan ya Kusini, wameiandikia familia ya Mungu nchini humo ujumbe wa matumaini, wakiitaka kusimama kidete kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa pamoja na kuhakikisha kwamba, Serikali ya Umoja wa Kitaifa inatekeleza dhamana na wajibu wake kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wananchi wa Sudan ya Kusini katika ujumla wake.

Maaskofu wanawataka wananchi kuondokana na woga usiokuwa na mashiko wala mvuto, tayari kushinda chuki na uhasama wa kikabila na kisiasa, ili kujenga misingi ya haki, amani, ustawi, mafao na maendeleo ya wengi. Umefika wakati wa kuondokana na falsafa ya jino kwa jicho inayoendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao na badala yake kuanza kujikita katika utamaduni wa amani, upendo na maridhiano kati ya watu. Maaskofu wanakumbusha kwamba dhana ya vita halali na ya haki imepitwa na wakati kwani vita haina macho wala pazia na kwamba, mwelekeo wa mafundisho ya Kanisa ni kujikita katika utamaduni wa amani inayosimikwa katika haki.

Maaskofu wanawataka wanasiasa kubomoa kuta zinazogumisha mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi ili kuanza ujenzi wa Sudan ya Kusini katika misingi ya umoja na mshikamano wa kitaifa. Utamaduni wa vita umepitwa na wakati, watu wanataka amani na utulivu, vichocheo vikuu vya ustawi na maendeleo ya watu. Ikumbukwe kwamba, vita inaendelea kuwaneemesha wafanyabishara haramu wa silaha ambao kamwe hawawatakii mema wananchi wa Sudan ya Kusini, wao daima wanataka kuona Sudan ya Kusini ikichafuka kwa damu ya watu wasiokuwa na hatia. Maaskofu wanakaza kusema, amani ni jina jipya la maendeleo Sudan ya Kusini!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.