2016-07-12 09:46:00

P. Lombardi, kisiki cha mpingu katika tasnia ya habari!


Padre Federico Lombardi, SJ, mwenye umri wa miaka 73 amekuwa ni gwiji katika tasnia ya habari ndani na nje ya Vatican. Lakini kuanzia mwaka 1990 hadi mwaka 2005 alikuwa ni mkurugenzi wa Vipindi Radio Vatican. Kuanzia mwaka 2005 hadi mwaka 2016 alikuwa ni Mkurugenzi mkuu wa Radio Vatican aliyeshuhudia mageuzi makubwa katika teknolojia ya habari na kuizamisha Radio Vatican katika mawimbi haya ya mageuzi makubwa.

Kunako mwaka 2001 hadi mwaka 2013 alikuwa ni Mkurugenzi mkuu wa Kituo cha Televisheni cha Vatican. Mwaka 2006 hadi mwaka 2016 alikuwa ni msemaji mkuu wa Vatican. Haya yote ni majukumu mazito na nyeti katika maisha na utume wa Kanisa, lakini Padre Federico Lombardi kwa moyo wa unyenyekevu, ujasiri, hekima na busara aliweza kutakeleza yote na hapo tarehe 31 Julai 2016 anang’atuka shughuli hizi na kuanza kufungua ukurasa mpya wa maisha yake kama Padre Myesuiti na Mwandishi wa habari.

Monsinyo Dario Edoardo Viganò, Mwenyekiti wa Sektretarieti ya Mawasiliano Vatican anasema, Padre Lombardi alikuwa na mtazamo mpana sana kuhusu maisha na utume wa Kanisa la kiulimwengu. Amekuwa ni Jaalimu makini wa tasnia ya habari kwa watu wengi; dhamana na utajiri mkubwa kwa kurugenzi ya mawasiliano ya jamii Sekretarieti kuu ya Vatican. Padre Lombardi anaacha urithi mkubwa wa taaluma na weledi wake unaojikita katika karama na mtazamo wa Kanisa la Kristo unaovuka mipaka ya utaifa, lugha, jamaa na tamaduni za watu.

Padre Lombardi katika utekelezaji wa majukumu yake alijikita katika kukuza na kudumisha umoja unaofumbata utofauti na hivyo kulitajirisha Kanisa la Kristo. Utajiri wa pili anasema Monsinyo Viganò ambao Padre Lombardi analiachia Kanisa ni kutaka kukuza na kudumisha umoja wa Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume. Kila mtu akichangia karama na mapaji ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa zima. Ni kiongozi ambaye ametekeleza dhamana na wajibu huu nyeti katika hali ya unyenyekevu mkubwa! Miaka 73 si haba anahitaji kujipumzishakutoka katika pilika pilika za maisha haya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.