2016-07-12 09:11:00

Dr. Burke, hii ni dhamana nyeti sana!


Dr. Greg Burke msemaji mkuu wa Vatican anayetarajiwa kuanza kutekeleza majukumu yake hapo tarehe 1 Agosti 2016 katika mahojiano maalum na Radio Vatican anasema amefurahishwa na uamuzi wa Baba Mtakatifu Francisko kumpatia dhamana ya kuwa ni msemaji wake mkuu, lakini anaichukua dhamana hii kwa woga na wasi wasi mkubwa kutokana na uzito wa kazi yenyewe. Kuwa Msemaji mkuu wa Vatican si kazi ya maji kwa glasi.

Dr. Greg anasema, kwa miaka yote hii amefurahia kufanya kazi katika tasnia ya habari, lakini uteuzi huu wa Baba Mtakatifu Francisko kuwa msemaji wake mkuu, ni dhamana nyeti. Baba Mtakatifu anaendelea kufanya mabadiliko katika Sekretarieti ya Vatican kwa kukazia umoja wa Kanisa unaofumbatwa katika Ukatoliki, ili kushirikishana tamaduni, lugha na karama mbali mbali ambazo Roho Mtakatifu analijalia na kuliwezesha Kanisa kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya familia ya Mungu.

Kanisa Katoliki ni moja, takatifu na la mitume. Kanisa linataka kuwafikia watu wengi zaidi kumbe, kwa karama na mapaji haya, linaweza kuwafikia watu kwa haraka zaidi. Kuna idadi kubwa ya waamini wa Kanisa Katoliki wanaozungumza Kiingereza na Kihispania, hawa pia wanapaswa kuwa ni walengwa wa ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa familia ya Mungu.

Dr. Greg Burke anampongeza na kumshukuru Padre Federico Lombardi, msemaji mkuu wa Vatican anayemaliza muda wake hapo tarehe 31 Julai 2016. Ni kiongozi ambaye ameonesha uvumilivu na uungwana mkubwa wakati akitekeleza dhamana na majukumu yake kama msemaji mkuu wa Vatican. Ni kiongozi ambaye amejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro na Kanisa la Kristo. Hizi ni karama ambazo anamwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kumkirimia anapoanza kuandika ukurasa mpya wa maisha na utume wake kama Msemaji mkuu wa Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.