2016-07-11 10:23:00

Patriaki mstaafu Twal anaishukuru familia ya Mungu!


Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Patriaki Fouad Twal wa Yerusalemu la kutaka kung’atuka kutoka madarakani kadiri ya sheria za Kanisa Namba 401 § 1. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu akamteuwa Mheshimiwa Padre Pierbattista Pizzaballa, O.F.M kuwa Msimamizi wa Kitume wa Upatriaki wa Yerusalemu pamoja na kumpandisha hadhi kuwa Askofu mkuu.

Patriaki Fouad Twal ameiandikia familia ya Mungu Yerusalemu barua ya shukrani na matashi mema, akionesha jinsi ambavyo wameweza kushirikiana kwa dhati kwa ajili ya kulihudumia Kanisa la Kristo; wakastahimili mateso na mahangaiko ya ndani pamoja na watu wote wenye mapenzi mema dhidi ya chuki na utamaduni wa kifo, kwa matumaini kwamba, iko siku mwanga wa Kristo Mfufuka utawang’aria na hivyo utu, haki na amani kutawala katika nyoyo za watu.

Kwa njia ya mateso na mahangaiko makubwa, Kanisa limeweza kukua na kukomaa kwani mkono wa Kristo Yesu uliweza kuwategemeza, wakasali na kuvumilia pamoja sasa umefika wakati wa kung’atuka kutoka madarakani. Anawashukuru waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema waliompokea kama mchungaji, kaka na mhudumu wao, wakashirikiana naye kwa sala na ibada mbali mbali.

Patriaki Twal anawakumbuka kwa namna ya pekee ndugu zake Wakleri na Watawa kutoka katika Mashirika mbali mbali waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani zao katika huduma ya elimu, afya na maendeleo endelevu. Anawashukuru wale wote aliobahatika kukutana nao katika huduma yake ya Kikuhani. Anawashukuru viongozi wa Makanisa, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki katika Nchi za Kiarabu na Baraza la Makanisa Mashariki ya Kati kwa ushirikiano na umoja waliomwonesha katika roho na ukweli.

Patriak Twal anamshukuru Mungu kwa Kanisa kuweza kupata Watakatifu wapya wawili kutoka katika Nchi Takatifu, kwa mfano wa karama, maisha na majitoleo yao, wawe ni mfano bora wa kuigwa na waamini katika hija ya maisha yao hapa duniani kuelekea kwenye Ufalme wa Mungu. Anang’atuka kwa mujibu wa Sheria za Kanisa, lakini ataendelea kuwasindikiza kwa sala na sadaka yake na anawataka kujenga upendo, umoja na ushirikiano kati yao. Anachukua nafasi hii kumpongeza Askofu mkuu mteule Pierbattista Pizzaballa aliyepewa dhamana ya kufanya maandalizi ya kumpata Patriaki mpya baada ya kusimamia maeneo matakatifu kwa muda wa miaka 12.

Patriaki Twal anaonesha historia ya familia ya Mungu katika Upatriaki wa Yerusalemu katika kusimama kidete kulinda na kudumisha misingi ya haki na amani; mambo yanayohitaji toba na wongofu wa ndani; sala na uwajibikaji, daima wakitegemea uaminifu wa neema ya Mungu, tayari kumpokea Patriaki ambaye atawekwa wakfu kwa ajili ya Kanisa la Mungu. Kanisa linahitaji kujipyaisha na kuendelea kushirikiana na Msimamizi wa Kitume kwa njia ya sala na upendo kwa kutambua kwamba, hakuna jambo lolote lisilowezekana mbele ya Mwenyezi Mungu, kwani daima anaendelea kufanya kazi pamoja na Kristo Yesu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa lake. Ili kazi ya Mungu iweze kuzaa matunda yanayohitajika kuna haja ya kujitakasa mbele ya Mungu, daima wakijitahidi kujisadaka kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa la Kristo katika imani, matumaini na unyenyekevu mkuu. Mwishoni, Patriaki mstaafu Twal anaikabidhi familia ya Mungu huko Yerusalemu chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa, akiwatakia amani na utulivu kutoka kwa Kristo Yesu. Anawaomba kumkumbuka pia katika sala zao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.