2016-07-11 14:59:00

Hija ya Papa Francisko nchini Georgia & Azerbaijan


Baba Mtakatifu Francisko anatarajia kufanya hija ya kitume nchini Georgia na Azerbaijan kuanzia tarehe 30 Septemba – tarehe 2 Oktoba 2016. Ratiba elekezi inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ataondoka kwenye Uwanja wa Kimataifa wa Fiumicino majira ya saa 3:00 za Asubuhi na kuwasili kwenye Uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Tbilisi majira ya 9:00 Alasiri. Baba Mtakatifu baada ya kupata mapokezi ya heshima atakwenda kumtembelea Rais na kuzungumza na viongozi wa Serikali, Kisiasa pamoja na Wanadiplomasia wanaowakilisha nchi zao huko Georgia.

Ratiba inaonesha kwamba Baba Mtakatifu pia atakutana na kuzungumza na Patriaki Ilia II pamoja na Patriaki mkuu wa Georgia kwenye Makao makuu ya Upatriaki wa Georgia. Baba Mtakatifu anatarajiwa kufunga siku ya kwanza ya hija yake ya kitume nchini Georgia kwa kukutana na kuzungumza na Jumuiya waamini wa Syria ya Wakaldea katika Kanisa la Mtakatifu Simoni.

Jumamosi tarehe 1 Oktoba 2016, Baba Mtakatifu ataadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Uwanja wa Michezo wa M. Meskhi, baadaye atakutana na kuzungumza na Wakleri pamoja na Watawa katika Kanisa la Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni. Papa pia atakutana na kuzungumza na wafanyakazi katika mashirika ya misaada ya Kanisa Katoliki mbele ya Kituo cha huduma cha Wacamilliani. Baadaye, Baba Mtakatifu atahitimisha siku kwa kutembelea Kanisa kuu la Svietyskhoveli lililoko Mskheta.

Jumapili, tarehe 2 Oktoba, 2016, Majira ya saa 2:10, asubuhi, Baba Mtakatifu anatarajiwa kuondoka kutoka katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Tbilisi kuelekea Azerbaijan anakotarajiwa kuwasili majira ya saa 3:30 kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa “Heydar Aliev” ulioko Baku. Hapo atapokelewa kwa heshima zote na baadaye kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa la Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili huko Baku, eneo linaosimamiwa na kuendeshwa na Wasalesiani. Baba Mtakatifu pamoja na ujumbe wake, watapata chakula cha mchana kwenye Jumuiya ya Wasalesiani. Baadaye yatafuata mapokezi ya kitaifa, huko kwenye Ikulu ya Genclik pamoja na kumtembelea Rais wa nchi.

Baba Mtakatifu Francisko atapata nafasi ya kuzungumza na viongozi wa Serikali na Waanasiasa katika Kituo cha “Heydar Aliyev”. Atakutana baadaye na kufanya mazungumzo ya faragha na Sheikh mkuu wa waamini wa dini ya Kiislam huko Caucus katika Msikiti mkuu wa “Heydar Aliyev”. Baadaye Baba Mtakatifu atakutana na kuzungumza na Askofu wa Kanisa la Kiorthodox na Rais wa Jumuiya ya Wayahudi. Baadaye saa 1: 15 jioni, Baba Mtakatifu ataondoka kurejea tena mjini Roma na kuwasili majira ya saa 4:00 Usiku kwa saa za Ulaya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.